Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo wa pili kutoka kulia akiwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) Michael Mjinja wa nne kutoka kulia pamoja na wadau wa gesi ya mitungi inayotumika majumbani (LPG) kutoka nchi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Tatu wa Afrika 2016 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo anayeelezea jambo, akiwa pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) Michael Mjinja wakiwa katika maonesho ya gesi hiyo ya mitungi inayotumika majumbani (LPG)
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) akiwa katika banda akipata maelezo kutoka kwa wadau wa LPG. Wengine katika picha ni Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake.
Na Rhoda James
Imeelezwa kuwa kuanzia mwezi Septemba mwaka huu Serikali itaanza Uagizaji wa Pamoja wa Gesi inayotumika Majumbani (LPG).
Hayo yalielezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo mwazoni mwa wiki wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa mwaka 2016 kuhusu masula ya Gesi ya Mitungi inayotumika majumbani kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Dkt. Pallangyo alisema kuwa lengo la mkutano huo lilikuwa ni kupata uzoefu kutoka kwa nchi zilizoendelea na pia kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo ikiwemo usambazaji, usalama na ujazaji wa mitungi hiyo.
Aliongeza kuwa, Uagizaji wa gesi hiyo ya mitungi (LPG) utafanywa kwa Pamoja lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kodi ya serikali inakusanywa ipasavyo kutoka kwenye Sekta hiyo na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hao hawamiliki soko hilo.
“Bei ya gesi ya mitungi inayotumika majumbani ni ghali, upatikaniji wake ni mgumu na pia haipatikani kwa mitungi midogo zaidi ambayo kila mwananchi wa kawaida anaweza kumudu,” alisema Pallangyo
Aliongeza kuwa, nishati hiyo inaleta ushindani ukilinganishwa na mafuta ya taa, na kutolewa mfano kuwa mafuta ya taa yanapatikana kwa urahisi na kwa viwango tofauti ambavyo mwananchi wa kawaida anaweza kununua kulingana na uwezo wake tofauti na ambavyo gesi inapatika na kwenye maduka makubwa na kwa bei ya juu. Na kuongeza kuwa ni vema gesi hiyo ya mitungi (LPG) ikapatikana kwa viwango vya kununulika na kwa bei nafuu.
“Ni vema wafanyabiashara wakubwa wa gesi hii ya mitungi (LPG) wakashirikiana na wafanyabiashara wadogo ili kukabili changamoto zilizopo kwenye sekta hii. Pia waangalie wapi kuna fursa hasa upande wa Afrika,” alisema Pallangyo.
Aidha, Dkt. Pallangyo alisema kuwa gesi hiyo ni muhimu kutokana na fursa nyingi na usalama wake, kutokana na utafiti wa Shirika la Afya Dunia (WHO) uliofanywa kuwa ikiwa nusu ya watu duniani wataitumia gesi hii ya mitungi (LPG) wataokoa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 900 kwa karne ijayo.
Pia, aliongeza kuwa utumiaji wa gesi hiyo ya mitungi imekua kwa kiasi kikubwa na kusema kuwa mwaka 2010 hadi 2011 tani 2,225 zilitumika ikilinganishwa na 2014 hadi 2015 tani 5,762 zilizotumika ongezeko ambalo ni kubwa.
Mkutano huo ulishirikisha washiriki kutoka nchi 33 mbalimbali wakiwemo waoneshaji (Exhibitors) kutoka sehemu mbalimbali duniani na ulifadhiliwa na kampuni za Oryx gesi na Hexagon Ragasco.
No comments:
Post a Comment