Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema imeanza kupokea malipo kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wa miaka ya nyuma.
Wadaiwa hao wameibuka ikiwa ni siku saba tu, tangu bodi hiyo itangaze kiama kwa wadaiwa wote sugu wa walionufaika na mikopo ya bodi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao kwenye vyombo vya habari, sambamba na kuunda tume ya kuwasaka wadai hao.
Aidha, Bodi hiyo imeanza rasmi kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria, kwa kuwatembelea kwenye ofisi zao kwa ajili ya kukagua na kuwahakiki ili kuweza kubaini, kama wamewasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB.
Akizungumza na Gazeti la Habari Leo kwa njia ya simu Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema kwa sasa mwitikio wa wanufaika kuanza kulipa madeni yao ni mkubwa ikilinganishwa na siku za nyuma.
“Ukweli ni kwamba, mwitikio ni mkubwa, wengi wanajitokeza kulipa, wiki iliyopita tulikuwa na idadi ya wanufaika takribani 42,000 waliokuja kulipa lakini hadi leo (jana) wameongezeka na kufikia 45,000 na wanaendelea kuongezeka,” alisisitiza Badru.
Kuhusu kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa wanaoendelea kutokulipa, mkurugenzi huyo alisema bado mchakato wa kutekeleza azma hiyo, unaendelea na kwa sasa bodi hiyo inafuatilia kwanza taratibu za kisheria kuhusu jambo hilo.
“Suala hili lina masuala kama mawili au matatu yanayohusu masuala ya kisheria kwa hiyo, linashughulikiwa na kitengo chetu cha sheria baada ya hapo tutawaambia lini tunaanza kuchapisha majina na picha za wadau hawa sugu,” alisema.
Aidha Badru alizungumzia hatua ya kuwabana waajiri, Badru alisema tayari timu maalum ilishaundwa na imeanza kazi ya uhakiki katika ofisi za waajiri hao, ingawa hakutaja ofisi hizo kutokana na sababu za kiutendaji.
SIKILIZA WAPO RADIO FM 98.1 KWA HABARI NA MATUKIO SANJARI NA VIPINDI VINGINE
SIKILIZA WAPO RADIO FM 98.1 KWA HABARI NA MATUKIO SANJARI NA VIPINDI VINGINE
No comments:
Post a Comment