Sunday, January 22, 2017

WANANCHI JIMBO LA DIMANI, ZANZIBAR WAPIGA KURA KWA AMANI NA UTULIVU.

Hatimaye wananchi wa Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga leo wamejitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali kupiga kura kumchagua Mbunge atakayewawakilisha kwa kipindi cha miaka miaka 4.
Zoezi la upigaji wa Kura katika vituo mbalimbali lilianza majira ya saa 1 asubuhi  likifanyika kwa hali ya Amani na Utulivu huku baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura wakipongeza maandalizi mazuri yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzine (NEC)  kufanikisha Uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa, Mhe. Semistocles Kaijage akizungumza kuhusu mwenendo wa Uchaguzi huo mara baada ya kutembelea vituo  vya kupigia kura katika jimbo hilo na  kuzungumza  na Mawakala wa Vyama vya Siasa waliokuwepo vituoni, Waangalizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wa Uchaguzi  huo amesema Tume imeridhishwa na kazi nzuri  iliyokuwa ikiendelea katika vituo mbalimbali vya kupigia Kura. 
Wananchi wakiangalia majina yao kabla ya kupiga kura katika kituo cha Bweleo katika jimbo la Dimani leo.
“ Viongozi wa Tume tumetembelea vituo mbalimbali vya kupigia Kura katika jimbo la Dimani; tumeona wenyewe upigaji wa Kura unaendelea vizuri, tumewauliza Mawakala, Watazamaji na Wasimamizi wa Vituo vya Uchaguzi  kila mmoja amesema Uchaguzi unakwenda vizuri, nachoweza kuwaambia watanzania Uchaguzi Dimani unakwenda Vizuri” Amesema Jaji Kaijage.
Amesema Wasimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo hilo wanaendelea kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili pia kushughulikia kwa haraka changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika  baadhi ya vituo vya kupigia Kura.
Ameeleza kuwa zoezi zima la upigaji wa Kura linaendeshwa kwa uwazi mkubwa, Utulivu na Amani na kuwawezesha wananchi kupiga kura bila vikwazo vyovyote.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (Katikati) akizungumza na Msimamizi kituo cha Dimani Bi. Abdu Simai Haji leo wakati zoezi la upigaji kura likiendelea katika jimbo la Dimani.
Aidha, Mhe. Kaijage amebainisha kwamba endapo yatajitokeza malalamiko yoyote wakati zoezi la upigaji wa Kura likiendelea katika vituo mbalimbali , Mawakala wa Vyama vya Siasa ambao ni wasimamizi wa Maslahi ya Wagombea na Vyama vyao Vituoni watajaza fomu  ya malalamiko  Na. 14 kwa mujibu wa Sheria ambayo inatoa fursa ya kushughulikiwa kwa malalamiko hayo.
Aidha, amebainisha kuwa mara baada ya zoezi la upigaji wa kura kumalizika leo saa 10 jioni kazi ya kuhesabu Kura itafuata ili hatimaye wamnanchi wa Jimbo la Dimani waweze kupatiwa matokeo ya maamuzi waliyoyafanya kupitia Kura zao.
Mhe. Kaijage amesisitiza kuwa Wasimamizi wote wa Uchaguzi huo wamepewa mafunzo ya kuzingatia ili kuhakikisha wanaendesha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa na kuwezesha matokeo kutangazwa kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kumjua mshindi wa Uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (wa pili) akiwa ameambatana na Baadhi ya Watendaji wa NEC na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Bi. Idaya Selemani Hamza (wa Kwanza) akiwasili katika kituo cha Kupigia Kura cha Kombeni katika jimbo la Dimani kuangalia maendeleo ya Upigaji wa Kura leo.

“ Endapo taratibu zote za Uchaguzi zitakuwa zimekamilika kwa mujibu wa Sheria, hakutakuwa na sababu yoyote ya kuchelewesha matokeo,mpaka sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi tumeridhishwa na mwenendo mzima wa zoezi la upigaji wa Kura na matokeo yatatolewa kwa wakati” Amesisitiza.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe akizungumzia zoezi la Upigaji wa Kura amesema kuwa Wapiga Kura wanaoruhusiwa kupiga kura ni wale waliokidhi Sifa na Vigezo vilivyoainishwa kisheria kuwawezesha kupiga Kura.

Amesema  kwa mujibu wa Sheria Msimamizi wa Kituo ndiye mwenye mamlaka ya maamuzi katika kituo cha kupigia Kura ikiwa ni pamoja na kuamuru kuondolewa kwa mtu yeyote atakayeonekana kufanya fujo au kuzuia zoezi la uchaguzi kuendelea kituoni.

Katika Uchaguzi Uchaguzi huo mdogo wa Ubunge wa jimbo la Dimani jumla ya Wapiga Kura 9,280 wanatarajiwa Kupiga kura katika Vituo 29 huku vyama vya Siasa vyenye wagombea vinavyoshiriki Uchaguzi huo ni 11 huku Waangalizi wa Uchaguzi waliojitokeza kushiriki katika Uchaguzi huo ni zaidi ya 300.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (Katikati) akizungumza na waandishi wa Habari wa Zanzibar kutoa tathmini ya hali ya Uchaguzi mara baada ya kuetembelea vituo mbalimbali vya kupigia kura katika jimbo la Dimani leo.
Baadhi ya Wangalizi wa Uchaguzi katika jimbo la Dimani wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Dimani leo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (Kushoto) akizungumza na Mawakala wa Vyama vya Siasa waliokuwepo ndani ya kituo cha kupigia Kura cha Kombeni katika jimbo la Dimani leo. Wengine wanaochukua taarifa ni Watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mmoja wa Wananchi katika jimbo la Dimani akipiga Kura yake kumchagua Mbunge katika jimbo la Dimani leo. Picha na Aron Msigwa –NEC.

No comments:

Post a Comment