Friday, January 27, 2017

JAFO AAGIZA KUPIGWA MARUFUKU SHUGHULI ZA KIBINADAMU KWENYE VYANZO VYA MAJI KONGWA.

MARU

Naibu Waziri wa Nchi OR TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo akikagua ujenzi wa daraja katika barabara ya Mbande, Sejeli, Matuge inayokwenda hadi Kiteto yenye urefu wa kilomita 57 wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
MARU 1
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo akitathmini ujenzi wa daraja katika barabara ya Mbande, Sejeli, Matuge hadi Kiteto wilayani Kongwa mkoani Dodoma alipofanya ziara wilayani humo, aliyesimama mbele kulia kwake ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Kongwa Bw. Ngusa Izengo.
MARU 2
Naibu Waziri wa Nchi OR TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo (Mb) akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Kongwa alipofanya ziara ya kushtukiza.Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Kongwa Bw. White Zuberi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Kongwa Bw. Ngusa Izengo
MARU 3
Naibu Waziri wa Nchi OR TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo (Mb) akiwapa pole na kujitambulisha kwao baadhi ya Wagonjwa waliokwenda kupata matibabu hospitali ya wilaya ya Kongwa alipofanya ziara katika hospitali hiyo.
MARU 4
Naibu Waziri wa Nchi OR TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo (Mb) akipata maelezo ya baadhi ya vifaa vya upimaji toka kwa Mganga Mkuu wa wilaya Kongwa (DMO) Dkt Festo Mapunda katika alipofanya ziara katika hospitali ya wilaya Kongwa kujionea hali ya utendaji na changamoto zinazowakabili watumishi na wagonjwa.
…………
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Kongwa kufanya ukaguzi kwenye vyanzo vya maji na kupiga marufuku shughuli za kibinadamu zinazofanyika ili kuokoa vyanzo hivyo kukauka.
Kauli hiyo ilitolewa katika ziara aliyoifanya wilayani humo alipokuwa akizungumza na  watumishi na madiwani.
Jafo amesema kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo za kilimo zinatishia vyanzo vya maji kukauka huku kukiwa hakuna jitihada za wataalam kunusuru hali hiyo.
Amefafanua kuna mlima unaitwa Mlima wa Mongo una chemchem kwa miaka ya nyuma kulikuwa na msitu mkubwa lakini kwasasa watu wamelima hadi mlimani, hivyo kuna kila sababu wataalam kupita kuzuia shughuli hizo juu ya milima.
“Maji yaliyokuwa yakija Chamkoroma yanakuja Suguta hadi Mang’weta kwasasa hali si hivyo, maji yamekauka vyanzo vyote vya maji watu wamefyeka na maafisa wapo. Tunazungumza sasa inawezekana miaka kumi ijayo hali ikawa mbaya zaidi ya sasa,”amesisitiza Jafo
Jafo amesema kwasasa upatikanaji wa maji kwenye wilaya hiyo ni ya kubahatisha kutokana na hali hiyo na inawezekana kuna maeneo maafisa misitu wanashirikiana na watu vyanzo kuharibika.
Ameagiza kulindwa kwa vyanzo vya maji ili kuepuka kuingiza Kongwa kwenye balaa kubwa la ukame.
Hata hivyo, amesema utendaji wa kazi wa Mhandisi wa maji utapimwa kulinga na utatuzi wa matatizo ya maji kwenye wilaya hiyo.
 “Injiani wa maji unafanya nini kuhakikisha Kongwa inakuwa na maji yanapatikana?, tunataka utumie taaluma yako kuhakikisha maji yanapatikana hatutaki watu wa kukaa tu ofisi wanalala.Kongwa hali si shwari,”amesema
Amesema kuna umuhimu wa mtaalam wa maji kufanya kazi kujibu kero za wananchi na kuongeza hali ya upatikanaji wa maji kutokana na wilaya hiyo kukua.
Katika hatua nyingine, Jafo amewataka watendaji wa wilaya hiyo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uaminifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Amesisitiza watumishi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ili kuleta maendeleo kwenye wilaya hiyo huku akiwataka wakuu wa idara kuacha kukaa maofisini na badala yake waende kwa wananchi ili kuwatatulia kero zinazowakabili.
Kadhalika, Naibu Waziri huyo ametoa miezi mitatu kwa wilaya hiyo kuhakikisha inaweka Genereta katika Hospitali ya wilaya hiyo ili kuweza kukabiliana na tatizo la umeme kukatika mara kwa mara.
Naye, Mhandisi wa maji wa Wilaya hiyo,Salim Bwaya amesema  upatikanaji wa maji kwasasa ni wastani wa asilimia 47.5  na ni kwa mgao kutokana na vyanzo vya maji vilivyopo havitoshelezi.

MARU

No comments:

Post a Comment