Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar
es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba (kushoto) na Mkurugenzi wa Ajira
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw.
Ally Msaki wakisaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali na
Taasisi hiyo utakaowezesha vijana kupata mafunzo ya uzalishaji wa mazao
ya ngozi katika Taasisi hiyo Kampasi ya Mwanza ili kuchochea uchumi wa
viwanda nchini.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar
es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba (kushoto) akibadilishana hati ya
makubaliano ya ushirikiano na Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu, Bw.Ally Msaki (kulia), makubaliano hayo ni kati ya Taasisi hiyo
na Serikali ili kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya uzalishaji wa mazao
ya ngozi.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar
es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba (kulia) akifafanua kwa waandishi
wa Habari kuhusu mikakati ya taasisi hiyo kushiriki katika ujenzi wa
uchumi wa viwanda kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na stadi
zinazoendana na mahitaji ya soko. Kushoto ni Meneja Rasilimali Watu na
Utawala wa DIT Bw. Sebastian Ndahani.
Mkurugenzi Msaidizi
anayeshughulikia Taarifa za Soko la Ajira Bw.Ahmed Makbel toka Ofisi ya
Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu akieleza umuhimu wa
vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali katika kuwajengea uwezo
ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda. Kushoto ni
Mkurugenzi wa Ajira, Bw. Ally Msaki kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu
Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Baadhi ya waandishi wa habari
wakiwa kwenye picha ya pamoja na wataalamu wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) mara baada ya
Taasisi hiyo kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano kati yake na
Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Picha na Frank Mvungi (MAELEZO)
………………………………………………………………….
Na Fatma Salum-MAELEZO
Serikali imepanga kutumia bilioni
15 kuwapatia vijana stadi za kazi zitakazowawezesha kujiajiri na
kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini
Dar es salaam wakati wa kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano kati
ya Taasisi ya Teknolojia Dar es saalam (DIT) na Serikali kupitia Ofisi
ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Akizungumzia makubaliano hayo
Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Bw. Ally Msaki amesema kuwa yatasaidia kuiwezesha Taasisi
hiyo kutoa mafunzo kwa vijana hasa ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na
ngozi ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“Vijana 1000 wataanza kupata
mafunzo mwezi Februari mwaka huu na yatakayohusu utengenezaji wa bidhaa
za ngozi na program hii ipo ndani ya mpango wa miaka mitano.” Alisema
Msaki.
Mafunzo hayo ya stadi za kazi kwa
vijana yatagharimiwa na Serikali na yatahusisha vijana walio katika
mfumo rasmi na wale wasio katika mfumo rasmi wa elimu lengo likiwa ni
kuwakwamua vijana ili washiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Akifafanua Msaki alisema kuwa
dhamira ya Serikali ni kuwawezesha vijana baada ya mafunzo hayo
kujiajiri na kuwaajiri wenzao hivyo kuondokana na tatizo la ajira na
kuongeza nguvukazi ya taifa kwenye uzalishaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi
ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba alibainisha kuwa
Taasisi hiyo imejipanga vyema kuwawezesha vijana kwa kutoa mafunzo
yanayoendana na mahitaji ya soko na kuweka msisitizo katika mafunzo kwa
vitendo.
Taasisi ya Teknolojia Dar es
salaam (DIT) ipo imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya
Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati.
No comments:
Post a Comment