Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (katikati) akizungumza na vikundi vya wanawake na vijana kutoka katika Jiji la Arusha kabla ya Kukabidhi hundi za Mikopo ya robo ya kwanza na ya Pili kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo amefungua mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vinavyokopeshwa na kutoa mikopo kwa vikundi 85 vya wanawake na vikundi 40 vya vijana kutoka katika kata zote za Jiji la Arusha.
Akikabidhi hundi zenye thamani ya Sh Mil 624 kwa vikundi hivyo ikiwa ni mikopo ya robo ya kwanza na ya pili kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Mhe. Gambo amewataka kinamama na vijana kutumia fedha hizo kwa shughuli zilizokusudiwa ili ziweze kuleta manufaa na kuwatoa katika lindi la umasikini.
“Mikopo hii inatolewa ili kuendeleza shughuli za kijasiriamali ambazo ndizo zilizopelekea mkidhi vigezo vya kupata Fedha; Nimatumaini yangu fedha hizi zitawawezesha kuongeza mitaji yenu na kuwapa ari ya kujituma zaidi huku mkizingatia nidhamu ya pesa ili muweze kuzirejesha kwa wakati na makundi mengine waweze kupata fedha hizo”Alisema Rc Gambo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(Katikati) akikabidhi hundi ya Tsh Mil 425 kwa wawakilishi wa Wanawake Bi. Mariamu Okash(Kata ya Kati) na Rose Charles(Kata ya Olorieni).
Aliongeza kuwa tofauti na mikopo hii ya halmashauri baada ya kuwawezesha vijana waendesha boda boda kwa kuwapatia Pikipiki 200 kundi litakalofuata ni wakinamama ambao watanufaika na Fedha zitakazorejeshwa na vijana hao kwa kupewa mitaji midogomidogo kadiri ya uhitaji.
Aidha Rc Gambo alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji kuunda timu maalumu ya kuchunguza utoaji wa Mikopo kwa Kipindi cha Miaka mitatu kama ilifuata taratibu, vikundi vilivyonufaika kama ni hai na hali ya urejeshaji.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Kalisti Lazaro Bukhay ambaye alishiriki katika zoezi la utoaji mafunzo na kukabidhi hundi amesema Kikundi ambacho hakitarejesha fedha zote za mkopo ama kuchelewesha marejesho kwa namna yeyote ile hakitapatiwa mkopo katika mwaka unaofuata ila wale watakaofanya vizuri katika biashara zao na kukuza mitaji wataongezewa kiasi cha kukopa kulingana na hali ya shughuli zao.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Mrisho Gambo akikabidhi hundi ya Tsh Mil 199 kwa wawakilishi wa Vijana Amos Kosani (Daraja II) na Janeth Prosper (Kata ya Unga Ltd).
Mikopo hiyo inayotolewa kwa mujibu wa Sheria na miongozo inayoelekeza asilimia kumi ya Mapato ya ndani ya Halmashauri kutolewe kama Mikopo ya riba nafuu kwa vikundi vya wananwake na vijana na kwa jiji la Arusha kiasi kinachotakiwa kutolewa ni Bil 1.2 kwa Mwaka huu wa Fedha hivyo kiasi kilichotolewa ni kwa kipindi cha nusu mwaka.
Fedha hizo zinatolewe kwenye Saccos au Vicoba vyenye nguvu katika Kata husika ili kurahisisha usimamizi na urejeshaji wa mikopo hiyo. Hivyo Saccos na Vicoba ndizo zinazokopesha vikundi vilivyoainishwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) kwa riba ya asilimia 10 na wao hubaki na asilimia 8 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na kurejesha Halmashauri riba ya asilimia 2 tu.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Eng. Gaston Gasana (kwanza kulia) akitoa taarifa fupi ya Utoaji wa Mikopo ya Wananwake na Vijana kwa robo ya kwanza na ya Pili kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 kwenye hafla ya kukabidhi hundi za mikopo hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqarro(Kwanza kushoto) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo kukuabidhi hundi kwa vikundi vya Wanawake na Vijana wa Jiji la Arusha.
Vikundi vya Wanawake na Vijana kutoka Kata mbalimbali za Jiji la Arusha wakimskiliza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (hayupo Pichani) kabla ya kukabidhiwa Mikopo inayotokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani.
No comments:
Post a Comment