WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini kuwa tayari kwenda kufanya kazi kokote watakakopangiwa na Serikali kulingana na mahitaji ya eneo husika.
Amesema moja ya wajibu wa watumishi wa umma ni kuwatumikia na kuwahudumia Watanzania sehemu yoyote walipo ili kuwaletea maendeleo na atakayeshindwa ni vema akatafuta shughuli nyingine nje ya ajira za Serikali.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Septemba 23, 2016) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Mkunguni wilayani Mafia.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.
Waziri Mkuu alisema kila awamu inakuwa na mkakati wake, watumishi wa umma wanatakiwa kubadilika na kufanya kazi kutokana na awamu iliyoko madarakani inavyotaka
“Hii ni awamu ya kazi zaidi. Hata kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli ya hapa kazi tu! si neno la kufurahisha bali lina malengo yanayowataka Watanzania wote wafanye kazi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mganga Mkuu wa mkoa wa Pwani, Dk. Beatrice Byarugaba kuimarisha huduma katika hospitali ya wilaya ya Mafia na kupeleka madaktari bingwa ili kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata huduma nje ya wilaya hiyo.
Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kuimarishwa kwa kitengo cha (TEMESA) kwa kupeleka mafundi watakaomudu kufanya matengenezo ya magari wilayani huko ili kupunguza gharama za kusafirisha magari hadi makao makuu ya mkoa wa Pwani kwa matengenezo pale yanapohitaji matengenezo.
“Namna nyingine mnayoweza kufanya ni kuomba kibali maalumu cha kuruhusiwa kufanya matengenezo ya magari hayo kwenye karakana za watu binafsi zenye mafundi wenye sifa zinazotambulika na Serikali ili badala ya kuyapeleka Kibaha kwa matengenezo,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Ndikilo ameiomba Serikali kuipa kipaumbele hospitali ya wilaya hiyo yenye kuhudumia wananchi zaidi ya 50,000 ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa wataalamu, dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
“Kwa wilaya ya Mafia mgonjwa anapokosa dawa au vipimo maana yake aende Dar es Salaam au Rufuji au Mkuranga kufuata huduma hizo. Jambo hili linawagharimu sana wananchi hasa wa hali ya chini. Naiomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alitaja changamoto nyingine inayowakabili wananchi wa wilaya hiyo kuwa ni usafiri wa majini kutokuwa na uhakika kutokana na kukosekana kwa meli rasmi ya abilia yenye usalama na staha.
Alisema kwa sasa wananchi wengi wanasafiri kwa kutumia majahazi na boti ndogo ambazo si salama na kwa sababu hiyo aliiomba Serikali kutafuta namna ya kutatua tatizo hilo linaloikabili wilaya hiyo kwa muda mrefu.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mafia Shaib Nnunduma alisema wilaya hiyo inakabiliwa na upungufu wa watumishi 469 katika kada za afya, elimu barabara, maji na utawala.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, SEPTEMBA 24, 2016
No comments:
Post a Comment