Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi
Kasiga
Serikali imesema kuwa inashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo kuhakikisha kuwa madereva wanaoendesha magari aina ya malori ambao
wametekwa nyara jana na waasi wa kikundi cha Maimai katika eneo la Namoyo jimbo
la Kivu kusini katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanapatikana
wakiwa salama.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa kitengo cha
Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi
Kasiga leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
juu ya juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwakoa watanzania waliotekwa
nyara.
“Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na
Serikali ya Kongo inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha madereva hao
wanaachiwa huru haraka iwezekanavyo na kurudishwa nchini wakiwa salama”
“ Waasi hao wa Maimai wametoa masaa 24 hadi
kufikia leo wawe wamelipwa kiasi cha Dola 4,000 kwa kila dereva ili waweze
kuwaachia huru na kutishia kuwadhuru endapo hawatapata fedha hizo, hivyo basi
Serikali imeendelea kuwa na mazungumzo na Serikali ya Kongo ili kupata ufumbuzi
wa suala hili” alisema Kasiga.
Aliongeza kuwa malori yaliyotekwa nyara ni 12
kati ya hayo nane ni mali ya mfanyabiashara wa kitanzania Bw. Azim Dewji na
mengine ni mali za wafanyabiashara kutoka nchini Kenya.Aidha, Serikali
imewataka watanzania kufahamu hali ya usalama wa nchi wanazokwenda ili
kujikinga na matatizo mbalimbali yanayoweza kuwapata wakiwa katika nchi hizo.
No comments:
Post a Comment