Wednesday, September 21, 2016

TAARIFA YA JESHI LA POLISI KUTOKA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI

index
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-

KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI [GONGO]
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtu mmoja mkazi wa Sinde Jijini Mbeya aliyefahamika kwa jina la SIFA KYEJO (41) akiwa na pombe ya moshi [gongo] ujazo wa lita 20.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 20.09.2016 majira ya saa 08:00 asubuhi katika msako uliofanyika huko Mtaa wa Ilolo – Janibichi, Kata ya Sinde, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya. Upelelezi unaendelea
KUPATIKANA NA MICHE YA BHANGI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wawili waliofahamika kwa majina ya1.  ROZALIA KAYANGE (27) Mfanyabiashara na 2. SIKUZANI MWAMLIMA, (37) Mfanyabiashara wote wakazi wa mtaa wa Ndola  wakiwa wamepanda miche 2 ya bhangi uani nyumbani kwao.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 20.09.2016 majira ya saa 08:00 asubuhi katika msako uliofanyika huko Mtaa wa Ndola – Mbalizi, Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya.
Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya pia linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatii sheria za usalama barabarani. Aidha kumekuwa na tukio 01 la ajali ya kifo kama ifuatavyo:-
AJALI YA KIFO.
Mnamo tarehe 20.09.2016 majira ya saa 21:10 usiku huko Kijiji cha Mwakaganga, Kata ya Ubaruku, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya vumbi  kutoka Rujewa kwenda Ubaruku, Pikipiki yenye namba ya usajili T.744 CTB aina ya Sanlg ikiendeshwa na dereva mwanaume asiyefahamika, umri kati ya miaka 30  hadi 35 iliacha njia na kisha kuanguka na kusababisha kifo cha mwendesha pikipiki huyo papo hapo.
Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Serikali Wilaya ya Mbarali. Upelelezi unaendelea.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Kumekuwa na tukio 01 la mauaji kama ifuatavyo:-
MAUAJI.
Mtu mmoja mkazi wa Kijiji cha Ikubo Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya aliyefahamika kwa jina la KALI MWABUKUSI (56) alikutwa ameuawa kwa kupigwa mawe na wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi kisha mwili wake kutupwa kando ya Mto Lufilyo.
Mwili wa marehemu ulikutwa mnamo tarehe 20.09.2016 majira ya saa 07:00 asubuhi ukiwa umetelekezwa kando ya Mto Lufilyo huko Kijiji cha Ikubo, Kata ya Luteba, Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.
Inadaiwa kuwa watu hao walimvizia marehemu akiwa amelala peke yake kwenye nyumba ya dada yake aitwae FEDA KATEBA kisha kumchukua kwa nguvu umbali wa mita 250 kisha kumpiga hadi kufa.
Chanzo ni kipigo kilichotokana na imani za kishirikina kwani inadaiwa kuwa marehemu alikuwa anatuhumiwa kuwa ni mchawi kijijini hapo na alikwenda kujificha kwa dada yake siku hiyo kwa usalama wake.
Watuhumiwa wanne wamekamatwa kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo ambao ni 1. GOLDEN KAMBINGWE (45) Kaimu VEO – kijiji cha Ikubo 2. EDWARD KASTO (58) Mwenyekiti kijiji cha Ikubo 3. PHILIPO GONAGA (36) Mkazi wa Ikubo na 4. ANDEKENYE SIELA (72) Balozi wa Nyumba kumi wa eneo hilo. Upelelezi unaendelea.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria. Pia Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuacha kuamini ushirikina kwani una madhara makubwa katika jamii. Aidha anaendelea kutoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuwa makini hasa kwa kufuata na kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoepukika.
Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments:

Post a Comment