Wednesday, September 21, 2016

MAHAKAMA KUU YA TANZANIA KANDA YA DAR IMETUPILIA MBALI KESI YA MBUNGE WA ZAMANI WA JIMBO LA TEMEKE HILO, ABBAS MTEMVU WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM),

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar imetupilia mbali kesi ya mbunge wa zamani wa jimbo la Temeke , Abbas Mtemvu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), dhidi ya mbunge wa sasa wa jimbo, Abdallah Mtolea wa Chama cha Wananchi (CUF).
Uamuzi huo uliotolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Issa Maige, aliyekuwa akisiliza kesi hiyo, baada ya kuridhika na hoja za Mtolea aliyekuwa akiwakilishwa na Wakili Mohamed Tibanyendela na Mwanasheria wa Chama hicho, Hashim Mzirai.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Maige alisema kuwa madai ya Mtemvu aliyekuwa akiwakilishwa na mawakili Egid Mkoba na Samson Mbamba hayana mashiko kwa kuwa hata kama kungekuwa na kasoro alizokuwa akizilalamikia, basi zisingeweza kuathiri matokeo ya uchaguzi hivyo.

Hivyo jaji Maige alimthibitisha mbunge Mtolea kuwa mbunge halali wa jimbo hilo aliyechaguliwa kihalali, huku akimtaka Mtemvu kumlipa mbunge huyo gharama za kuendesha kesi hiyo.


Jaji Maige alisema kuwa madai ya Mtemvu kuwa Mtolea alipata kura tofauti na zile zilizotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi si kweli kwa kwa tofauti ya kura kati yao ni zaidi ya kura 5000.

Jaji Maige alisema kuwa hata kama Mtemvu angepewa kura za vituo alivyokuwa akidai kuwa matokeo yake hayakujumlishwa ambazo hazizidi 1800, bado zisingempa ushindi.

Akizungumzia madaia ya  kutokuwepo kwa fomu namba 21B Jaji Maihe alisema kuwa ushahidi wa shahidi wa Mtemvu ulikuwa na kasoro nyingi na kwmaba hata hivyo ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ni wa vituo vinane, ambapo hata hivyo hakuonesha walipata kura ngapi na viliathiri vipi Mtemvu kutokutangazwa mshindi.

Akizungumzia hukumu hiyo, Mtolea alisema kuwa mahakama hiyo imetenda haki kwa kuthitisha kile wananchi wa Temeke alichokiamua.
Mtolea alisema kuwa baada ya hukumu hiyo anawaahidi wananchi wa Temeke kuwa sasa atahakikisha anafanya kazi kwa nguvu zake na utashi wake wote kuijenga Temeke na kuiletea maendeleo bila kujali tofauti ya itikadi za kisiasa.

Mawakili wa Mtolea, Tibanyendelea na Mzirai walisema wakizungumzia hukumu hiyo walimshukru JajI Maige kuwa alitenda haki kwa kuzingatia maamuzi ya wananchi wa Temeke waliyoyafanya mwaka 2015 katika uchaguzi huo.

Mtemvu ambaye alikuwa akitetea nafasi yake kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa 2015, alifungua kesi mahakamani hapo akipinga matokeo yaliyompa ushindi Mtolea, akidai kuwa yeye ndiye aliyekuwa mshindi na kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alibadilisha matokeo yake akampa Mtolea.  

Mwisho

No comments:

Post a Comment