Na Ally Daud-Maelezo,Dar es Salaam.
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imetenga Tsh. Bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba, ukarabati wa majengo ununuzi wa vifaa katika jengo la upasuaji na jengo la wagonjwa mahututi (ICU).
Akizungumza hayo wakati Wa hafla fupi ya kuwaaga madaktari watakaosafiri kwenda nchini India Septemba 25 mwaka huu Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wa MNH Prof. Lawrence Museru alisema mradi huo unatarajia kuanzia Januari mwaka 2017.
"Tumetenga Bilioni 3.4 ili kuweza kuongeza na kukarabati vyumba vya upasuaji kutoka 12 hadi kufikia vyumba 20 pamoja na kuongeza vyumba vya ICU vinne na vitanda 40 pamoja na vifaa vipya ili kutoa huduma bora" alisema Prof. Museru.
Aidha Prof. Museru alisema kuwa hospitali hiyo pia inatarajia kuwapeleka nchini wataalamu 7 wakiwemo madaktari bingwa wa fani za pua, koo na masikio ili kujifunza kwa njia ya vitendo jinsi ya kufanya upasuaji na upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa watu wazima na watoto.
Prof. Museru aliongeza madaktari hao wanaenda kuhudhuria mafunzo ya mwezi mmoja katika hospitali ya Appolo iliyopo nchini humo ili kupunguza gharama ya za kusafirisha wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Akifafanua zaidi Prof. Museru alisema kuwa tayari hospitali hiyo imepeleka timu ya wataalamu 18 India ili kupata uwezo wa upandikizaji figo ambapo mafunzo hayo yanatarajiwa kukamilika miwshoni mwa mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu Wa Idara ya Pua na Masikio wa Hospitali hiyo, Dkt.Edwin Liombo alisema kuwa mafunzo hayo yakikamilika watakuwa wameokoa zaidi ya asilimia 50 ya gharama za upasuaji na upandikizaji wa masikio, pua na figo.
Aidha Dkt. Liombo aliongeza kuwa gharama za kupandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja ni kati ya Tsh. milioni 80 hadi Tsh. Milioni 100 na kiasi cha Tsh. Milioni 40 hadi 60 ikiwa ni gharama za kupandikiza figo kwa mtu mmoja nje ya nchi.
MWISHO
No comments:
Post a Comment