Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kuungana ili waweze kupata fursa katika miradi mikubwa ya ujenzi itakayoanza hivi karibuni hapa nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina endelevu ya 26 ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, Prof. Mbarawa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa na itatoa kipaumbele kwa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi watakaoungana ili kuwa na nguvu ya kutekeleza miradi hiyo kwa viwango.
“Tunao mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa miundombinu ya kisasa mjini Dodoma, ujenzi wa makazi ya kisasa ya wananchi, vyote hivi vinahitaji wataalamu walioungana, wenye nguvu ya kufanya kazi kwa haraka na ubora unaokubalika”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
3
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wadau wa sekta ya ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi wakati wa Ufunguzi wa Semina ya 26 ya Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi, Jijini Dar es salaam.
Ameitaka Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kujitangaza na kuwatangaza wataalamu wake ili huduma zao zitumiwe na wananchi wa ngazi zote kwa gharama nafuu.
“Shirikianeni na vyuo vinavyofundisha fani yenu ili viongeze udahili wa wanafunzi na kuhakikisha kazi zenu zinafanywa kisasa na kwa kuzingatia teknolojia”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameitaka Bodi hiyo kutoa elimu ya kutosha ili kuvutia wanafunzi wengi kupenda kusoma fani hiyo na wale wanaofanya vizuri wawape motisha ya kuwasomesha katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.
1
1
Msajili wa Bodi ya Usajili ya Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi (AQRB) Arch.Jehad Abdallah akisoma taarifa ya utekelezaji wa Bodi hiyo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa ufunguzi wa Semina ya 26 ya Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi, Jijini Dar es salaam.
Akizungumza katika semina hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya AQRB, Mbunifu Majengo Ambwene Mwakyusa, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Bodi yake imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata ramani za nyumba kwa bei nafuu ili kuwa na jamii yenye makazi ya kisasa.
Naye Msajili wa Bodi ya AQRB, Mbunifu Majengo Jehad Jehad amesema takribani Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi 1,333 pamoja na kampuni za fani hiyo 372 zimesajiliwa na zinatoa huduma kwa mujibu wa sheria za fani hiyo.
Amebainisha kuwa Bodi yake imejipanga kuhakikisha maadili ya taaluma hiyo hapa nchini yanalindwa na atakayekiuka atafutiwa usajili na kuadhibiwa kwa mujibu wa taratibu ya bodi hiyo.
Zaidi ya miradi ya ujenzi 1,963 imekaguliwa na bodi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha mwaka wa 2015 lengo ikiwa ni kuhakikisha ujenzi wowote unaofanyika nchini unakuwa na viwango bora.
2
2
Mwenyekiti wa Bodi wa bodi ya Usajili ya  Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi (AQRB) Arch. Ambwene Mwakyusa akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa ufunguzi wa Semina ya 26 ya Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi, Jijini Dar es salaam.
6
6
Washiriki wa Semina ya 26 ya Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi wakimsiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, (hayupo pichani) wakati wa semina hiyo jijini Dar es salaam.
7
7
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa bodi Bodi ya Usajili ya Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi (AQRB) mara baada ya ufunguzi wa Semina ya 26 ya wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi jijini Dar es salaam.(Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchuzi na Mawasiliano).