Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameitaka Bodi mpya ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) aliyoizindua leo jijini Dar es Salaam, kushughulikia kikamilifu changamoto zilizoko katika Tume hiyo.
Prof. Ndalichako ameiambia bodi hiyo kuwa amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kuhusiana na vyuo wanavyosoma, hivyo ni wakati wa bodi hiyo kufuatilia kwa ukaribu malalamiko hayo na kuyafanyia kazi.
“Tunaelewa kwamba wanafunzi ni watu wa kulalamika kila wakati, lakini yapo malalamiko ambayo yana tija na ni lazima yatatuliwe, kwa mfano malalamiko yanayohusu uvurugaji wa matokeo au taratibu zinazokuwa kandamizi kwa wanafunzi na walimu wa vyuo vikuu,” alifafanua Prof. Ndalichako.
Akitolea mfano wa taratibu kandamizi katika vyuo hivyo, Prof. Ndalichako amesema kwamba mwanafunzi anapopoteza kitabu cha chuo hulipishwa mara tatu ya gharama ya kitabu hicho huku mwanafunzi huyo akiwa ni mtoto wa masikini hali inayopelekea wanafunzi kutoazima vitabu wakihofia kulipishwa gharama kubwa pindi vitabu hivyo vitakapopotea.
Vile vile amesema kuwa kuna baadhi ya vyuo vimekuwa vikiwataka walimu kutoa taarifa ya kuacha kazi miezi mitano kabla ya kuacha kazi ambapo sheria mama inamtaka mwajiriwa kutoa taarifa ya kuacha kazi kwa mwajiri miezi mitatu kabla ya kuacha kazi.
Aliendelea kwa kusema kuwa taratibu hizo zinawakandamiza walimu kwani chuo kinapoamua kumfukuza kazi mwalimu humfukuza papo kwa hapo bila kumpa muda wa kujiandaa.
Pia amesema kuwa amepokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Ifakara mwezi Mei mwaka huu kuhusiana na walimu wa chuo hicho kuvuruga matokeo yao, lakini chuo hicho akijatoa maamuzi juu ya walimu hao mpaka hii leo, hivyo kuwaacha wanafunzi kuendelea kubaki nyumbani bila kujua hatima yao.
Aliongeza kwamba TCU inamamlaka yote yakuvifuatilia vyuo vikuu vyote nchini pamoja na kuangalia utendaji kazi wa vyuo hivyo ikiwa unaendana na viwango vilivyowekwa.
Aidha, ameitaka TCU kufanya utafiti wa wanafunzi walioko vyuoni ili kubaini wanafunzi wasio na sifa kutokana na baadhi ya vyuo kuingiza wanafunzi kinyemela bila kupitia TCU au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Vile vile, Prof Ndalichako ameitaka Bodi hiyo kutunga sheria ya Vyuo Vikuu itakayoipa meno tume hiyo kusimamia vyuo vikuu bila kuwa na pingamizi lolote.
Bodi hiyo itafanyakazi kwa kipindi cha miaka 3, kuanzia Septemba 28 mwaka huu hadi Septemba 2019, ikiongozwa na Mwenyekiti Prof. Philip Jacob Mtabaji.
No comments:
Post a Comment