Thursday, October 06, 2016

WAKURUGENZI WATAKIWA KULIPA POSHO ZA SARE KWA WAUGUZI


Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu,akiongea na wauguzi(hawapo pichani)wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 44 wa wauguzi Tanzania.

Wauguzi toka mikoa mbalimbali nchini wakimsikiliza waziri wa afya wakati wa mkutano huo,ambapo kwenye hotuba yao waliomba kulipwa posho na malimbikizo ya sare za wauguzi kiasi cha shilingi 120,000/=
Rais wa Chama cha Wauguzi Tangania(TANNA) Paul Magesa akimkabidhi zawadi ya shukrani kwa kushiriki nao Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,WZee na Watoto

Wakati watanzania wakiendelea kuchanga fedha na mahitaji mengine kwa waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera,Wauguzi waliohudhuria mkutano huo nao walichanga kiasi cha shilingi 4,196,500/= na kumkabidhi Waziri Ummy Mwalimu ili afikishe mchango wao na pole kwa mkoa huo(picha na Catherine Sungura,WAMJW)
Wakurugenzi wa halmashauri na wale wa hospitali za umma nchini wamepewa siku sitini kuanzia jana wawe wamewalipa posho za wauguzi za kununua sare za kazi ya shilingi laki moja na elfu ishirini pamoja na malimbikizo ya sare hizo.
Agizo hilo limetolewa mkoani hapa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 44 wa wauguzi Tanzania.
Waziri Ummy alisema asilimia themanini ya kazi zote  kwenye sekta ya afya nchini zinafanywa na wauguzi,hivyo aliwataka wakurugenzi  kuzingatia miongozo iliyopo ya Serikali, “kama mwongozo ni kulipa elfu thelatini lipa thelathini si  vinginevyo. Serikali imekwishatoa waraka wa kazi za ziada yaani “extra duty circular” ambao unapaswa kufuatwa hata mnapofanya kazi usiku kwani kuna masaa ya ziada”. 

“Nawaagiza waajiri wote kuzingatia nyaraka hizi ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima, Hili ni suala muhimu kwani mnakuwa kazini siku tano hadi sita kwa wiki hivyo mnahitaji sare walau tano ili muweze kubadilisha kila mara. Serikali itatoa waraka wa si chini ya laki tatu kulingana na hali ya uchumi itavyokuwa. Natumaini waraka huu utatoka mapema na kuanza kutumika mwaka ujao wa fedha hivyo kwa mwaka huu tuendelee kutumia waraka uliopo. 

Aidha, aliagiza baada ya siku sitini alizotoa kupatiwa orodha  za halmashauri ambazo hazitokuwa zimewalipa posho hizo na mikoa ipi”kwani kuna wauguzi wangapi hadi mshindwe kuwapa posho za sare ,mnataka wauguzi hawa waje kazini wawe wamevaa nini?aliuliza Waziri

Akijibu tatizo la kusimamishwa na kufukuzwa kazi kwa wauguzi na wakunga alisema ,suala la kusimamisha au kumwachisha kazi mtumishi lina taratibu zake ambazo zinapaswa kufuatwa. “Napenda kuliagiza Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania kuwaelimisha waajiri kuhusu hatua za kufuata katika kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi ili yaweze kusikilizwa kwa utaratibu zilizopo bila ya kuwaonea pande zote, Ni kweli kuwa unapoadhibiwa bila kosa inavunja moyo, Naomba ieleweke kuwa sio nia ya Serikali kuwaumiza wauguzi bali lengo letu kubwa ni kuondoa kero za wananchi ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia watumishi wote wazembe na wasiofuata maadili ya kazi”.
Hatahivyo Waziri huyo ametoa rai kwa jamii kuweza kuwaheshimu wauguzi na wakunga kwani kumtukana na kumnyanyasa ni kutomtendea haki kwani wauguzi wanatakiwa kupendwa na kuthaminiwa”wahenga walisema usitukane mkunga na uzazi ungalipo,hivyo wananchi msiwatukane wauguzi kwani mkeo au mtoto wako atajifungua na atasaidiwa na huyo mkunga,tuwapende na kuwaheshimu wauguzi”.
Aliwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuweka namba maalumu za wananchi kutoa malalamiko na kwa upande wa viongozi kuondoa urasimu wa kushughulikia malalamiko hayo kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuwashughulikia ambayo yamezidi na yanakatisha tamaa  kwa kada hiyo.

Kuhusu upungufu mkubwa wa wauguzi Waziri Ummy alisema ni kweli kuwa, nchi  inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa wauguzi hali inayopelekea muuguzi mmoja kuhudumia wagonjwa wengi zaidi ya uwezo wake,Mazingira hayo yanaweza kuathiri ubora wa huduma wanayotoa. 

“Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha watumishi wa afya wenye weledi wa kutosha wakiwamo wauguzi wanapatikana na kupangiwa katika vituo vya kazi sehemu mbalimbali za nchi yetu, Napenda nitumie fursa hii kuwahakikishia kuwa Serikali imepanga kuongeza idadi ya wauguzi nchini kila mwaka mara tu zoezi la kuwaondoa watumishi hewa kukamilika ninaamini Sekta ya Afya itapewa kipaumbele cha kwanza katika ajira mpya. Hivyo, niwaombe muendelee kuwa wavumilivu na kutoa huduma vema kwa kuzingatia taaluma yenu wakati jitihada za kuongeza watumishi zikiendelea”. 


Wauguzi nchini wamekuwa na utaratibu wa kukutana kitaifa na kuelimishana juu ya maadili,majukumu ya viongozi wa chama katika utoaji wa huduma za afya kwa weledi kwa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.Mkutano umebeba ujumbe maalumu na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi :nguvu ya mabadiliko,uboreshaji wa uthabiti wa mfumo wa afya.

No comments:

Post a Comment