Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu (kulia) akimkaribisha Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge (kulia) alipomtembelea ofisini kwake leo mjini Bukoba kujionea uharibifu wa miundombinu ya sekta ya maji iliyosathiriwa na tetemeko la ardhi.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kagera Mhandisi Avitus Exavery akimuonesha Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge uharibifu wa tanki la maji la shule ya sekondari ya Ihungo uliosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera mapema Septemba 2016.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge (wa nne kulia) akitembelea miundombinu ya maji iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera mapema Septemba 2016.
Baadhi maungio ya maji yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera mapema Septemba 2016.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge (kulia) akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu (kulia) leo mjini Bukoba kujionea uharibifu wa miundombinu ya sekta ya maji iliyosathiriwa na tetemeko la ardhi.
…………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba.
Serikali imeanza kurekebisha miundombinu ya maji iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera ili kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama waweze kuendelea na kazi zao za kawaida za kila siku.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ofisini kwake leo mjini Bukoba kujionea uharibifu wa miundombinu ya sekta ya maji iliyosathiriwa na tetemeko la ardhi.
“Ni lazima turudishe miundombinu ya maji ambayo imeharibiwa na tetemeko la ardhi ili kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama, maji wanaweza kuyapata lakini yanaweza kuwa si salama, ni kukumu langu kuja kupita ili niweze kukagua kujua baada ya tetemeko hili bado maji ni salama au kuna mambo ya kufanya ili tuweze kuyashughulikia” alisema Waziri Mhandisi Lwenge
Katika kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Kagera wanapata maji ya uhakika, Waziri Mhandisi Lwenge amesema kuwa ziara yake inalenga pia kuhakikisha azma ya Serikali ya kuwapatia wananchi maji ya uhakika.
Mpango huo wa Serikali unalenga kuwapatia wananchi waishio mijini maji kwa kiwango cha asilimia 95 ambapo kwa wananchi waishio vijijini wanapata maji ya uhakika kwa asilimia 85 ifikapo 2020.
Kwa wananchi waishio vijijini, Waziri Mhandisi Lwenge amesema kuwa kwa sasa wananchi wanapata maji kwa asilimia 60 hadi 70 wakati kwa ngazi ya kitaifa inaonesha wananchi hao wanapata maji kwa asilimia 72.
Kwa upande wa sekta ya umwagiliaji, Waziri Mhandisi Lwenge amesema kuwa hali ya mvua nchni inazidi kupungua mwaka hadi mwaka.
Waziri Mhandisi Lwenge amesema kuwa ili kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha, Serikali pamoja na wananchi kuweka nguvu kwenye kilimo cha umwagiliaji ambacho ndio chenye uhakika wa kutatua changamoto ya uhaba wa chakula na upatikanaji wa maji.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Waziri Mhandisi Lwenge amsema kuwa Serikali imeanzisha Tume ya Umwagiliaji na kuainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ikiwemo mkoa wa Kagera ambayo yanaweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji.
Hatua hiyo ya Serikali itasaidia kujengwa kwa miundombinu ambayo itawasidia wananchi wanaoishi katika maeneo ya umwagiliaji waweze kufaidika kwa kilimo cha umwagiliaji ambayo ndio azma ya Serikali.
Waziri Mhandisi Lwenge amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 kuwa na hekta milioni 1 za kilimo cha umwagiliaji ambapo kwa sasa zinalimwa hekta 461,0000 ambayo ni sawa na asilimia 1.6 ya eneo lote ambalo linaweza kutumika kwa umwagiliaji na kuutaja mkoa Kagera ni moja wapo ya maeneo ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Zaidi ya hayo, Waziri Mhandisi Lwenge amesema kuwa kulingana na jiografia ya mkoa wa Kagera, upo uwezekano wa kujenga mabwawa ambayo yatatumika kwa kilimo cha umwagiliaji, kufuga samaki, maji ya kunyweshea mifugo na kuweka rasilimali maji ambayo nchi nyingi duniani zimeanza kutegemea kilimo hicho ili kujihami na upungufu wa mvua.
Akimkaribisha Waziri Mhandisi Lwenge, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu amesema kuwa katika sekta ya maji mkoani humo, miundombinu ya maji imeathirika na kuharibiwa na tetemeko la ardhi na kusababisha upatikanaji wa maji kwa wananchi kuwa si wa kuridhisha.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amemhakikishia Waziri wa maji na umwagiliaji kuwa maagizo na maelekezo yake aliyoyatoa yatasimamiwa na kutekelezwa ili kuwahudumia wananchi na maisha yao yaweze kuwa bora na kujiletea maendeleo.
Katika ziara yake mkoani Kagera, Waziri Lwenge ametembelea maeneo miundombinu ya maji yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi, Mamlaka ya Maji Safi na Salama Bukoba, chanzo cha maji cha Bunena pamoja na tanki la maji la shule ya sekondari Ihungo lililoathiriwa tetemeko la ardhi.
No comments:
Post a Comment