Thursday, November 03, 2016

MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM ANATARAJIWA KUPANDA KIZIMBANI NOVEMBA 9 MWAKA HUU 2016

Image result for PICHA YA PAUL MAKONDA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  Novemba 9,2016 anatarajiwa kupanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujitetea dhidi ya kesi ya madai ya Sh 200 milioni  iliyofunguliwa na waliokuwa makada wa CCM, Mgana Msindai na John Guninita.
Siku hiyo, Makonda anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Seneni Mponda atatoa ushahidi wa  utetezi wake mbele ya Hakimu  Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Kwa upande wa Msindai na Guninita wao wanatetewa na mawakili kutoka kampuni ya Uwakili ya BM, Benjamin Mwakagamba na Ester Shedrack.

Katika kesi hiyo ya madai namba 68 ya 2015, Msindai na Guninita kupitia wakili wao, Mwakagamba walifungua kesi wakiiomba Mahakama hiyo ya Kisutu kumuamuru Makonda awaombe msamaha na kumlipa kila mmoja wao kiasi cha Sh 100 milioni.
Wanadai viasi hivyo vya fedha kutokana na maneno ya kuwadhalilisha yaliyotolewa na Makonda wakati akiwa Katibu uhamasishaji chipukizi CCM alipoitisha mkutano na waandishi wa habari.
Pamoja na hayo, wanaiomba mahakama hiyo, itoe zuio  la kudumu kwa Makonda  asizungumze  tena maneno ya kashfa dhidi yao wala kuyasambaza kama alivyofanya awali.
Pia wanaomba Makonda kulipa riba pamoja na gharama za kesi  na nafuu nyingine.
Walidai kuwa Makonda  wakati akiwa Katibu uhamasishaji chipukizi wa CCM,  katika mkutano wake alitoa maneno akidai kuwa Msindai na Guninita ni vibaraka vibaraka wanaotumiwa tumiwa kuharibu chama cha CCM kwa nguvu ya pesa.
Msindai na Guninita wanadai maneno hayo yaliyotolewa na Makonda  yamewadhalilisha na kufanya waonekane ni viongozi ambao hawafai kuongoza CCM na kwamba yamewadhalilisha mbele ya jamii na CCM kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment