Thursday, November 03, 2016

Image result for picha ya tundu lissu
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kumkamata Mbunge wa Singinda Mashariki kupitia Chadema,Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi pamoja na Wahariri wa gazeti la Mawio.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alifikia hatua hiyo  baada ya Lissu kutoonekana mahakamani na mdhamini wake Robert Katula kueleza amekwenda kusikiliza kesi Mwanza.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Simba alihoji ni kwanini Lissu hakuiomba mahakama ruhusa  na ni kwa sababu gani maudhurio yake  mahakamani yamekuwa ni matatizo?
Wakili wa Serikali, Patrick Mwita aliiambia mahakama kuwa kabla ya kuendelea na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka kuna rufaa ambayo washtakiwa wameikata katika kesi hiyo, mahakama Kuu.
Kutokana na Lissu kutoonekana mahakamani hapo, Wakili huyo wa Serikali, Mwita aliiomba mahakama itoe hati ya kumkamata.
Hakimu Simba,  alisema Lissu angetumia busara kuomba ruhusa ya mahakama, kuna misingi ya busara tungeiangalia pengine, “Hati ya kumkamata itolewe”na hakuna msamaha.
Pia alitoa samasi kwa wadhamini wa Lissu Novemba 21,2016 kufika mahakamani kujieleza ni kwanini wasilipe fungu la dhamana walilolisaini wakati wa kumdhamini Lissu.
Awali mahakama hiyo iliwaonya wadhamini hao wa Lissu,  Ibrahimu Ahmed na Robert Katula kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha anafika mahakaman wakati wote anapohitajika.
Ni baada ya kujieleza kuwa Lissu hakufika mahakamani hapo kwa sababu amekwenda nje ya nchi kwa matibabu, ni afisa wa mahakama na mbunge hivyo hawezi kuruka dhamana na kwamba atakaporejea watahakikisha anafika mahakamani.
Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa Lissu ni afisa wa mahakama ni vema angefuata masharti ya dhamana  na kwamba  hati yake ya kusafiria iwasilishwe mahakamani na awe anaomba kibali cha mahakama kusafiri nje ya nchi.
Wakili wa Lissu, Peter Kibatala  alidai kuwa kila mtu ana haki ya kuaminiwa, wadhamini  wametoa taarifa kwa wakati na akaihakikishia mahakama kuwa Lissu anaiheshimu mahakama na utaratibu wake na kwamba hali hiyo haitajirudia na atakaporejea ataomba msamaha kwa kilichotokea.
Kabla, Hakimu Simba alimtaka Lissu kufika mahakamani hapo kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana baada ya yeye pamoja na wadhamini wake kutokuwepo mahakamani hapo kama sheria inavyotaka.
Upelelezi wa kesi hiyo umekwisha kamilika, Washtaki wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na  Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob,.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
 Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam,  walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Mehboob  anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala,  Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.
Alidai mshtakiwa huyo pia  alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya  sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
Mbali na mashtaka hayo washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016,  Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar   wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

No comments:

Post a Comment