Mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump amelishambulia shirika la uchunguzi wa jinai nchini Marekani (FBI) kwa kumuondolea makosa minzani wake wa chama cha Demcratic Hillary Clinton siku moja kabla ya uchaguzi.
Mkurugenzi wa FBI James Comey ameliandikia bunge la Congress barua akisema uchunguzi mpya kuhusu barua pepe zilizopatikana hazikutoa ushahidi wa kulifanya shirika hilo kubadilisha msimamo wa awali, kwamba hakuna ushahidi wa kumfungulia mashtaka.
Maafisa kampeni wa Bi Clinton wamesema wamefurahia sana kwamba suala hilo hatimaye limetatuliwa.
Habari hizo ziliondoa wingu jeusi ambalo lilikuwa limegubika kampeni yake siku za mwisho mwisho kabla ya uchaguzi kufanyika.
Kura za maoni za karibuni zaidi ambazo matokeo yake yalitolewa Jumapili, kabla ya tangazo jipya la FBI, zilionyesha Bi Clinton anaongoza kwa alama nne mbele ya Bw Trump.
Lakini mgombea huyo wa Republican amelalamikia uamuzi wa shirika hilo.
Akiongea katika viunga vya mji wa Detroit, Bw Trump amesisitiza kwamba haingewezekana kwa FBI kuchunguza barua pepe ambazo zinakadiriwa kufikia 650,000 katika kipindi hicho kifupi.
"Kwa sasa tunashuhudia (Bi Clinton) akilindwa na mfumo wa ulaghai. Ni mfumo laghai kabisa. Nimekuwa nikisema hili kwa muda mrefu," alisema akiwa Sterling Heights, Michigan.
"Hillary Clinton ana makosa, mwenyewe anajua, na FBI wanajua, watu wanajua na sasa wajibu ni kwa watu wa Marekani kutoa haki kwenye debe la kura Novemba 8."
Ingawa Bi Clinton hakuzungumzia barua hiyo mpya ya mkurugenzi mkuu wa FBI kwenye mkutano wake wa kampeni, amekuwa akisisitiza kwamba ana imani ataondolewa makosa.
Akiongea mjini Manchester, New Hampshire, Jumapili Bi Clinton alisema taifa hilo linakabiliwa na wakati muhimu sana na lazima Wamarekani wachague kati ya "kugawanyika na umoja".
Mwezi Julai, FBI walisema alikosa kumakinika kwa kutumia sava ya kibinafsi kutuma barua pepe rasmi za kikazi alipohudumu kama waziri wa mambo ya nje kuanzia 2009-13, lakini haikumpata na makosa ya uhalifu.
Hata hivyo, siku 11 kabla a uchaguzi, Bw Comey alitikisa kampeni alipotangaza kwamba kumegunduliwa barua pepe mpya kumhusu Bi Clinton.
Hilo liliwakera maafisa wa kampeni wa Bi Clinton, lakini likampa matumaini Bw Trump ambaye kura za maoni zilikuwa zimeonyesha alikuwa nyuma ya mpinzani wake.
Lakini kwenye barua kwa Bunge la Congress James Comey alisema wachunguzi wa FBI walifanya kazi "usiku na mchana" kuchunguza barua pepe mpya, ambazo ziligunduliwa kwenye uchunguzi mwingine tofauti.
Zilipatikana kwenye laptopu ya mume wa zamani wa mmoja wa washauri wakuu wa Bi Clinton, mbunge wa zamani Anthony Weiner, ambaye anatuhumiwa kutuma ujumbe wa kimapenzi kwa msichana wa miaka 15.
Bw Comey amesema wachunguzi hawajapata sababu ya kubadilisha uamuzi wa wawali wa FBI kwamba Bi Clinton hafai kufunguliwa mashtaka.
Maafisa wa serikali wameambia vyombo vya habari Marekani kwamba wachunguzi wamebaini kwamba barua pepe zilizopatikana zilikuwa za kibinfasi au zilikuwa nakala za barua pepe ambazo tayari walikuwa wamezitathmini awali.
Wagombea wote wawili wanatarajiwa kufanya kampeni za dakika za mwisho katika majimbo yanayoshindaniwa Jumatatu.
Bi Clinton ataanza siku yake Michigan, ngome ya Democratic ambayo imeangaziwa sana na Bw Trump siku za karibuni.
Baadaye ataelekea Philadelphia ambapo ataungana na Rais Barack Obama, Michelle Obama, Bill Clinton na Bruce Springsteen.
Mgombea huyo wa Democratic atakamilisha kampeni yake ya kuingia ikulu ya White House kwa kampeni ya "jitokezeni mkapige kura" katika jimbo la Carolina Kaskazini.
Bw Trump ataelekea Florida, North Carolina na Philadelphia kabla ya kufunga siku kwa mkutano wa kampeni Grand Rapids, Michigan.
Katika majimbo ambayo upigaji kura mapema unaruhusiwa, Wamarekani karibu 42 milioni wamepiga kura za urais.
Wamejitokeza kwa wingi katika majimbo muhimu yanayoshindaniwa sana kama vile Florida, Carolina Kaskazini na Nevada.
Katika uchaguzi mkuu wa 2012, takriban wapiga kura 126 milioni walijitokeza na kupiga kura.
No comments:
Post a Comment