JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
Ndugu Wananchi,
Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwamo kisukari,
magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kansa na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa
kwa sasa yamekuwa yakiongezeka kwa kazi zaidi hapa nchini. Magonjwa haya huchangia
zaidi ya asilimia hamsini ya mzigo wa magonjwa duniani kwa vile husababisha
gharama kubwa za matibabu, ulemavu na hata vifo.
Siku
ya Kisukari Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 14 ya Mwezi
Novemba. Siku hii ilianza kuazimishwa rasmi mwaka 1991 na mashirika mawili ya kimataifa ya
International Diabetes Federation [IDF] na World Health Organization [WHO]
baada ya kuona ugonjwa wa kisukari unaongezeka sana duniani kote. Ilipendekezwa
tarehe 14 ya mwezi Novemba kila mwaka kwa sababu ndio siku ya mwanasayansi
maarufu Sir Frederic Banting alipozaliwa na ndiye mgunduzi wa dawa ya Insulin
na alikuwa wa kwanza kuitumia kwa wagonjwa wa kisukari.
Tanzania
kama zilivyo nchi nyingine zote Duniani inaadhimisha siku hii kwa kutoa elimu
ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara mbalimbali yatokanayo na ugonjwa
wa kisukari.
Ndugu Wananchi,
Ugonjwa
wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi
kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. Sukari hutumiwa na mwili ili kupata
nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji
kichocheo cha insulin. Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai
ili kutengeneza nishati lishe. Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo
hiki kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari
kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye
chembechembe hai za mwili.
Kama nilivyosema mwanzoni, watu wengi hawajitambui ya kuwa wana ugonjwa huu.
Wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema. Dalili za kisukari
ni rahisi kuzitambua nazo ni: kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua
uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu. Ukiwa na dalili mojawapo
kati ya hizi, wahi hospitali ukapime sukari.
Ndugu Wananchi,
Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa
kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania. Tafiti
za ugonjwa wa kisukari zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa 246
milioni duniani. Takwimu za mwaka 2015 kutoka kwenye
Atlas ya kimataifa ya Kisukari,zinaonyesha kuwa kulikuwa na wagonjwa milioni 415
duniani kote. Ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa
kuwa na wagonjwa milioni 642. Katika bara la Afrika kulikuwa na wagonjwa wa
kisukari milioni 14.2 mwaka 2015 na idadi hii itaongezeka na kufikia milioni
34.2. kwa Tanzania mpaka waka 2015 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 822,880 wa
kisukari.
Utafiti
uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini Tanzania ulionyesha ya
kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25-64 wana ugonjwa wa
kisukari.
Aidha
Nchini Tanzania takwimu za watoto wenye kisukari mwaka huu 2015 ni kati ya asilimia 15 mpaka 20 ya wagonjwa wote
wa kisukari ambao wanatibiwa kwenye kliniki nchini. Lakini wapo wengine wengi
hawajitokezi kwenye kliniki kwa sababu mbalimbali zikiwemo,imani potofu, gharama
pamoja numbali wa huduma za afya zilipo pamoja na ukosefu wa elimu juu ya
tatizo hili.
Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya
Kisukari Duniani mwaka 2016 ni “Macho
yote kwenye Kisukari”. Kauli mbiu hii inalenga katika kutufumbua macho zaidi
kwamba kisukari ni tatizo linalopamba moto siku hata siku hivyo tuongeze nguvu
katika kuhakikisha kwamba tunajikinga na tabia mbalimbali ambazo zinapelekea
upatikanaji wa tatizo hili ikiwemo asuala azima ya ulaji unaofaa, kufanya mazoezi,
kuepuka matuizi ya pobe kupita kiasi na matumizi ya tumbaku.
Ulaji
unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko cha kutosha kukua na kuwa na
uzito wa kawaida na chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini. Kwa mfano
vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto, protini husaidia
kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali,matunda, mboga, vitamin na
madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa.
Ndugu Wananchi,
Ulaji
usiofaa ni kula chakula bila kuzingatia aina na kiasi
kulingana na mahitaji ya mwili. Hii huweza kusababisha kupungua au kuzidi kwa
virutubishi mwilini. Ulaji usiofaa ni pamoja na kula vyakula vyenye mafuta
mengi hasa yale yatokanayo na wanyama, kula vyakula vyenye chumvi nyingi,
sukari nyingi, kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka na kutokula mbogamboga
na matunda kiasi cha kutosha. .
Kutofanya
Mazoezi ya mwili chakula
kinacholiwa kwa kawaida hutumika na mwili kufanya kazi mbalimbali. Iwapo
chakula hakitatumika hubadilishwa na kuhifadhiwa mwilini kama mafuta na hatimaye
husababisha uzito kuzidi. Mambo yanayochangia mwili kutotumia chakula kilicholiwa
ni pamoja na kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi ya mwili.
Uzito
na unene uliozidi uzito unakuwa
umezidi pale ambapo uzito wa mtu unakuwa asilimia 20 zaidi ya uzito unaotakiwa.
Ili kupima hali hiyo viashiria mbalimbali hutumika; njia inayotumika mara
nyingi ni ile ya uwiano wa uzito na urefu wa mwili kulingana na viwango maalumu
vilivyowekwa.
Msongo
wa mawazo huweza kusababisha
ulaji usiofaa na huweza kufanya mifumo mbalimbali ya mwili kutofanya kazi
vizuri.
Matumizi
ya pombe huchangia katika
kuongeza uzito mara nyingi. Unywaji wa pombe za aina zote huendana na ulaji wa
vyakula kwa wingi ambayo huchangia kuongeza uzito. Pombe yenyewe ikizidi uharibu
maini, kusababisha utapiamlo kwa wale wanaoishia kunywa pombe zaidi ya kula chakula.
Uvutaji
wa Sigara na matumizi ya bidhaa zitokanazo na Tumbaku licha ya kuwa ni matumizi
yasiyo na tija, tumbaku husababisha madhara mengi mwilini yakiwemo magonjwa ya
moyo na mishipa ya damu, saratani na magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Ndugu Wananchi,
Ili
kuzuia ugonjwa wa kisukari na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya
ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa
kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa
wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya. Madhara au
athari za ugonjwa wa kisukari ni upofu, mtoto wa jicho , retinopathy, shinikizo
la damu kuwa juu, stroke, ugonjwa wa figo, kupungua nguvu za kiume, upungufu wa
kinga mwilini, kuwa na vidonda hasa miguuni visivyopona pamoja na ganzi miguu au mikono.
Ndugu Wananchi,
Serikali
inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa huduma kwa
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo
kisukari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani ya nchi na wa kimataifa.
Aidha, serikali, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na taasisi zinaendelea
kuandaa na kurekebisha sheria, kanuni na taratibu zinazoimarisha uzuiaji na
udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Ndugu Wananchi,
Serikali
inaeendelea kuandaa miongozo na mikakati ya kisera kwa kushirikisha jamii
katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza,
ikiwemo kisukari. Serikali imeimarisha ushiriki wa sekta mbalimbali za umma na
za binafsi katika kukabiliana na vyanzo vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Ndugu wananchi,
Kwa
kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari, kuanzia mwaka 1993, kama ilivyo
Sera ya Taifa ya Afya inatoa msamaha kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia
gharama za matibabu na inajitahidi kwa uwezo wa bajeti yetu pamoja na wahisani
wetu kuhakikisha kuwa dawa muhimu zinapatikana. Kwa sasa watoto wote na vijana
chini ya miaka ishirini na minne walio na kisukari wanapata mahitaji yao yote
kupitia kliniki za kisukari zilizopo nchini.
Kuanzia
mwaka 2012, serikali pamoja na washirika wake inatekeleza mpango wa kuthibiti
ugonjwa wa kisukari nchini. Lengo ni kuwa na kliniki za kisukari hadi katika
ngazi ya vituo vyote vya afya.
Ndugu wananchi,
Tanzania
inaungana na mataifa yote duniani kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la
mwaka 2011 la kuhakikisha ya kuwa kuna mpango kabambe wa kuthibiti magonjwa
yasiyo ya kuambukiza. Nchi yetu inaungana na mataifa mengine kuhakikisha ya kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanapungua kwa
asilimia 25 ifikapo mwaka 2025 kwa kupitia mpango mkakati wa kitaifa wa miaka
mitano (2016-2020). Mpango mkakati huu ambao ulizinduliwa mwezi wa Oktoba mwaka
huu unaainisha mikakati mizito ya kukabiliana na magonjwa haya.
Ndugu
wananchi,
Kwa bahati mbaya, unaweza kuwa na ugonjwa huu kwa muda
mrefu bila kuwa na dalili nilizotaja hapo awali. Hata hivyo, jinsi sukari
inavyokuwa juu, inaharibu mishipa ya damu na ya fahamu, macho na kusababisha upofu, moyo na figo kushindwa kufanya kazi, na miguu
kufa ganzi hadi kuwa na vidonda, au kunyauka kwa kukosa mzunguko wa damu.
Hivyo ninatoa wito
kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima afya yake kwa kuwa ugonjwa
huu unaweza usionyeshe dalili yoyote mapema. Ni vyema kila mmoja akapima afya
yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya afya. Endapo utatambuliwa kuwa una
ugonjwa wa kisukari tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na
wataalam wa afya.
Kwa wale ambao
wameshajitambua kuwa na matatizo ya kisukari lakini hawatumii huduma za
afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao
na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa ya kisukari.
Zingatia kauli mbiu ‘’
Macho yote kwenye Kisukari’’,
tuhakikishe tunapima afya zetu kutambua kama tuna tatizo la kisukari au la.
PAMOJA TUNAWEZA.
ASANTENI
KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment