Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akizungumza huku akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa mpango wa TREEP katika uzinduzi huo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akielezea mikakati ya Serikali katika usambazaji wa umeme vijijini wakati alipokuwa akizindua mpango wa kupanua wigo wa upatikanaji wa umeme vijijini (TREEP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB)
Sehemu ya wakazi wa Kwedizinga wilayani Handeni mkoani Tanga wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa inatolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani ) katika uzinduzi huo
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga akielezea mpango wa kupanua wigo wa upatikanaji wa umeme vijijini (TREEP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kwenye uzinduzi huo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga (kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird (katikati) wakisaini makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa kupanua wigo wa upatikanaji wa umeme vijijini (TREEP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kwenye uzinduzi huo. Kushoto kabisa ni Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Innocent Luoga.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga (kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird (kushoto) wakibadilishana nakala ya makubaliano baada ya utiaji saini wake katika uzinduzi huo. Katikati ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Mwenyekiti wa Bodi wa Wakurugenzi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dk. Gideon Kaunda akielezea mpango wa TREEP katika uzinduzi huo.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird (kulia) akielezea mikakati ya Benki ya Dunia (WB) katika kuisaidia serikali katika usambazaji wa umeme vijijini. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Innocent Luoga.
Mkandarasi kutoka kampuni ya Future Century Limited ya Tanzania, Hellen Masanja (wa kwanza kulia) akielezea mafanikio ya kampuni yake katika usambazaji wa umeme vijijini katika uzinduzi huo. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimsikiliza mmoja wa wakazi kutoka katika eneo la Kwedizinga wilayani Handeni mkoani Tanga alipokuwa akiwasilisha maoni yake katika uzinduzi huo.
……………………………………………………………………………..
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amezindua mpango mkubwa wa umeme nchini utakaowezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa takribani kaya 500,000 katika maeneo mengi ya vijijini.
Uzinduzi huo uliofanyika katika eneo la Kwedizinga wilayani Handeni mkoani Tanga ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka Benki ya Dunia (WB), Ujerumani, Sweden, Norway, Uingereza na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), watendaji kutoka katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tanga, wabunge, madiwani na wananchi kutoka kutoka katika maeneo mbalimbali mkoani Tanga.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Profesa Muhongo alisema kuwa mpango huo ni wa kihistoria kwa kuwa utakuwa ni mkombozi kwa Tanzania kwani umeme utakaozalishwa utakuwa ni wa uhakika na kuwezesha nchi kupiga hatua kubwa kiuchumi na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Alisema kuwa, serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kubuni vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ikiwa ni pamoja na maji, jotoardhi, upepo, gesi, jua, makaa ya mawe lengo likiwa ni kuendana na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini
“ Tunataka kuhakikisha kuwa tunaendana na kasi ya ongezeko la miradi mipya ya umeme vijijini kwa kuhakikisha kuwa tuna vyanzo vipya vya uzalishaji wa umeme,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo aliendelea kusema kuwa serikali ina mpango wa kuzalisha umeme wa uhakika na kuuza wa ziada katika nchi jirani kama vile Kenya, Uganda, Zambia n.k
Wakati huo huo akielezea mpango huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alisema kuwa serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB) zilikubaliana kuanzisha mpango wa kupanua wigo wa upatikanaji wa umeme vijijini Tanzania ujulikanao kama Tanzania Rural Electrification Expansion Program;(TREEP) lengo likiwa ni kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana katika maeneo ya vijijini kwa bei nafuu.
Alieleza kuwa mradi huo wa miaka sita unaotarajiwa kukamilika mwaka 2022, fedha zake zinatokana na mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) wa Dola za Marekani milioni 200.
Aliendelea kufafanua kuwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 25 ambazo zinaratibiwa na Benki ya Dunia zilizotolewa kama msaada kupitia Programu ya Kuongeza Kasi ya Nishati Jadidifu kwa Nchi Zenye Kipato cha Chini (SREP), kati ya fedha hizo kiasi cha Dola za Marekani milioni tisa zimejumuishwa chini ya TREEP
Mhandisi Nyamo-Hanga, alifafanua kuwa lengo la mpango wa TREEP ni kuongeza kasi ya usambazaji wa miundombinu ya umeme vijijini ikiwa ni pamoja na miundombinu ya usambazaji na ya uzalishaji hasa wa nishati jadidifu vijijini.
Aliongeza kuwa mpango wa TREEP ni wa kwanza kabisa kutumia mfumo mpya wa Benki ya Dunia unaojikita kwenye utekelezaji wa matokeo.
Alitaja washirika wengine wa mradi huu kuwa ni pamoja na Serikali ya Norway, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden (Sida), Umoja wa Ulaya (EU), Idara ya Serikali ya Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) ambapo miradi yake yote itasimamiwa na REA.
Alisema kuwa mpango wa TREEP utajumuisha maeneo matatu ambayo ni pamoja na eneo la kwanza litakalohusisha katika kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme wa gridi ambapo kiasi cha Dola za Marekani milioni 151 zitatumika katika eneo hili.
Aliendelea kusema kuwa eneo la pili litajikita kuendeleza mifumo ya umeme nje ya gridi kwa kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa sekta binafsi ili kuendeleza miradi ya nishati jadidifu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shughuli za uzalishaji mali ambapo kiasi cha Dola za Marekani milioni 42 zitatumika.
Alisema eneo la tatu litalenga katika kuendelea kujenga uwezo wa kitaalam kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wizara ya Nishati na Madini pamoja na wadau wengine ambapo kiasi cha Dola za Marekani milioni 16 zitatumika.
Akielezea mafanikio yanayotarajiwa kupatikana kutokana na mradi wa TREEP, Mhandishi Nyamo-Hanga alisema kuwa kaya zisizopungua 500,000 hadi milioni 2.5 zitaunganishwa na umeme wa gridi na nje ya gridi ikijumuisha takribani kilomita 24,000 ya miundombinu usafirishaji na usambazaji.
“Takribani watu 310, 000 watafikiwa na huduma ya umeme kupitia mifumo ya nje ya gridi pamoja na upatikanaji wa vyanzo vipya ya umeme hali itakayopelekea mabadiliko makubwa ya kiuchumi,” alisema Mhandisi Nyamo-Hanga.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird aliipongeza serikali ya Tanzania katika juhudi zake za kupambana na umaskini kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha nishati ya uhakika ya umeme inapatikana kwa gharama nafuu.
Bird alisema nishati ya umeme ni muhimu hususan katika kipindi hiki ambapo serikali imejikita katika uchumi wa viwanda na kuongeza kuwa Benki ya Dunia ipo tayari kushirikiana na Serikali katika maeneo yote ili malengo yake yaweze kufikiwa.
Alisema kupitia mpango wa TREEP huduma za jamii zitaboreshwa ikiwa ni pamoja na shule na hospitali za kisasa na upatikanaji wa maji ya uhakika kwa kutumia pampu zinazotumia umeme.
No comments:
Post a Comment