Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi – Kisutu, Yohanne Yongolo ameihairisha kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Mhe Tundu Lissu hadi Septemba 6 mwaka huu ili kutoa uamuzi wa maombi yaliyoombwa na upande wa mshtakiwa.
Kesi hiyo imehairishwa leo Jijini Dar es Salaam na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo kutokana na kushindwa kufikia muafaka juu ya hoja iliyotolewa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala ya kuiomba Mahakama kuleta barua ya maelezo kutoka kwa Afisa wa Makosa ya Jinai wa Kanda ya Dar es Salaam (ZCO) kabla ya mashahidi wawili kutoka upande wa Jamuhuri kuongea.
“Naihairisha kesi hii hadi Septemba 6 ambapo tutatoa uamuzi kulingana na sheria kama Afisa wa Makosa ya Jinai wa Kanda (ZCO) anatakiwa kuja kutoa ushahidi au kama mashahidi hawa walioletwa na upande wa Jamuhuri wanajitosheleza”, alisema Yongolo.
Kwa upande wake Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala amesema kuwa maelezo kutoka kwa Afisa wa Makosa ya Jinai wa Kanda ni ya muhimu kabla ya mashahidi wawili kutoka upande wa Jamuhuri kuongea pia mshtakiwa hawezi kujitetea bila kupata maelezo kutoka kwa afisa huyo.
Naye Wakili wa Serikali Mkuu, Bernad Kongola amesema kuwa Afisa wa Makosa ya Jinai wa Kanda sio shahidi katika shauri hilo hivyo kisheria hawalazimiki kumleta afisa huyo kuja kutoa maelezo mbele ya mahakama.
Mnamo Juni 28 mwaka huu, Lissu aliongea maneno ya kichochezi muda mfupi baada ya kutoka kusikiliza shauri lake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Maneno hayo yalimsababishia kufunguliwa kesi ambayo inasikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Yohanne Yongolo.
No comments:
Post a Comment