Mkutano mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ulioketi jana jijini Dar es Salaam ulivurugika pasipo malengo ya mkutano huo kufanikiwa.Mkutano huo ulilenga kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa ngazi za juu pamoja na kujadili barua ya kujiudhuru na ya kutengua kujiudhuru ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba.
Kwa mujibu wa msemaji wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Tanzania bara, Ridhiwan Hassan Kilala inasemekana kuwa masilahi binafsi ndiyo chanzo cha kuvurugika mkutano huo.
Kilala ameuambia mtandao huu kuwa, kuna baadhi ya viongozi waandamizi kutoka Zanzibar wanania ya kukidhoofisha chama cha CUF bara ili kishamiri Zanzibar peke yake jambo linalopingwa na wajumbe wa bara na kwamba kitendo hicho ndiyo mzizi wa mgogoro uliotokea jana.
Kilala alisema “Mkutano uliaghirishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano huo Julius Mtatiro baada ya kutokea vurugu kati ya wajumbe Bara na Zanzibar mara baada ya wajumbe kutoka bara kutaka barua ya kujiudhuru Lipumba na ile ya kutengua kujiudhuru iletwe hadharani isomwe ili wajumbe wachanganue sababu za lipumba za kujiudhuru kwa maana kwamba ijulikane kama alistahili kujiudhuru kwa manufaa ya chama au la.”
“Katibu Mkuu Maalim Seif Sharifu Hamad alipotakiwa kuzileta barua hizo awali alikataa,lakini hapo baadae alizeleta ndipo wajumbe wa bara tulipohitaji lipumba awepo ili athibitishe kama kinachosomwa ni sahihi au kimeongezwa chumvi, ” alisema.
Kilala alisema kuwa baada ya Lipumba kuingia katika mkutano huo mgogoro ulianza ambapo upande wa Zanzibar walidai kuwa Lipumba alijiudhuru na kushinikiza uchaguzi ufanyike huku wajumbe wa Bara wakitaka barua ya kujiudhuru na ya kutengua kujiudhuru zisomwe ili wajumbe wafanye uchambuzi yakinifu kwa lengo la kujua kama uamuzi wake uliokuwa na manufaa kwa chama au la.
“Baraza lilimuagiza Maalim kuleta barua zote mbili ili zijadiliwe, wajumbe wa Zanzibar hawakutaka hizo barua zijadiliwe, baadae barua ziliposomwa ilibainika kuwa Maalim Seif alikuwa na nia ya kukiuza chama na pia lengo lake CUF ife bara ili ishamiri Zanzibar jambo liliopingwa na wajumbe wengi wa Bara ,” alisema Kilala ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kilombero.
Aliongeza kuwa hadi dakika ya mwisho kabla ya kikao kuaghirishwa, wajumbe wa Zanzibar walitaka uchaguzi ufanyike huku wa bara wakitaka barua zijadiliwe kwanza ili kujiridhisha kama Lipumba alijiudhuru kwa manufaa ya chama au kwa manufaa yake binafsi.
“Ukweli ni kwamba wajumbe wa bara wengi wanamtaka Lipumba arudi katika wadhifa wake. Jambo la muhimu linalotakiwa kufanywa ni kuketi pamoja na kufanya maridhiano ili muafaka upatikane na tuijenge taasisi imara, ” alisema.
Kilala aliongeza “Na tujue kuwa tunagawanyika kutokana na baadhi ya watu kuwa na mikakati ya kuruhusu chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitawale Bara na CUF kitawale Zanzibar, hiki kitu hakitawezekana.”
Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF Abdul Kambaya alise kuwa mmkutano utatangazwa hapo baadae mambo yakishakamilika.
No comments:
Post a Comment