Na Masau Bwire,
Mwalimu wa kike mwenye
umri wa miaka 25 wa Shule ya msingi Msigani, Kimala Manispaa ya Kinondoni
Jijini Dar es salaam ameuawa kwa kupigwa risasi siku ya Jumamosi saa 2 usiku!
Kamanda
wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es salaam, Kamishina
Msaidizi wa Polisi (ACP) Christopher Sprian Fuime amesema mwalimu huyo aliuawa
kwa kupigwa Risasi hiyo wakati akijiandaa kufunga kibanda chake cha biashara
kilichopo pembeni mwa uwanja wa Shule anayofundisha.
Kamanda
Fuime amesema, wauaji hao ambao walifika katika kibanda cha mwalimu huyo wakiwa
wamepakizana kwenye pikipiki, walivunja kioo cha kibanda hicho, mmoja mwenye
bastola akaingia ndani na kumpiga Risasi iliyomsababishia kifo papo hapo, kisha
wao kuondoka bila kuchukua kitu chochote!
Amesema
juu ya meza katika kibanda cha biashara cha mwalimu huyo kulikutwa shilingi
laki tatu, vocha za simu na simu kadhaa za mkononi ambazo hazikuguswa na watu
hao, hali ambayo inalifanya Jeshi la Polisi lishindwe kubaini kwa haraka mpaka
hapo uchunguzi utakapofanyika sababu za mauaji hayo.
Kamanda
Fuime amesema, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itahakikisha hakuna jambazi
anayepata ushindi na kufanya raia waishi kwa hofu katika nchi yao na kuongeza
kwamba, kutoa uhai wa mtu kwa ajili ya Mali, chuki na uhasama ni vitendo
ambavyo havitavumiliwa na Jeshi la Polisi, litapambana na watu wenye tabia
hizo, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola.
Aidha
Kamanda Fuime ametoa mwito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi
ili kuwezesha kupatikana na kukamatwa kwa watu hao na wahalifu wengine.