Sunday, February 28, 2016

MWALIMU WA KIKE WA SHULE YA MSINGI MSIGANI JIJINI DAR ES SALAAM AUAWA KINYAMA KWA KUPIGWA RISASI.

Na Masau Bwire,
Mwalimu wa kike mwenye umri wa miaka 25 wa Shule ya msingi Msigani, Kimala Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam ameuawa kwa kupigwa risasi siku ya Jumamosi saa 2 usiku!

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es salaam, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Christopher Sprian Fuime amesema mwalimu huyo aliuawa kwa kupigwa Risasi hiyo wakati akijiandaa kufunga kibanda chake cha biashara kilichopo pembeni mwa uwanja wa Shule anayofundisha.

Kamanda Fuime amesema, wauaji hao ambao walifika katika kibanda cha mwalimu huyo wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki, walivunja kioo cha kibanda hicho, mmoja mwenye bastola akaingia ndani na kumpiga Risasi iliyomsababishia kifo papo hapo, kisha wao kuondoka bila kuchukua kitu  chochote!

Amesema juu ya meza katika kibanda cha biashara cha mwalimu huyo kulikutwa shilingi laki tatu, vocha za simu na simu kadhaa za mkononi ambazo hazikuguswa na watu hao, hali ambayo inalifanya Jeshi la Polisi lishindwe kubaini kwa haraka mpaka hapo uchunguzi utakapofanyika sababu za mauaji hayo.

Kamanda Fuime amesema, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itahakikisha hakuna jambazi anayepata ushindi na kufanya raia waishi kwa hofu katika nchi yao na kuongeza kwamba, kutoa uhai wa mtu kwa ajili ya Mali, chuki na uhasama ni vitendo ambavyo havitavumiliwa na Jeshi la Polisi, litapambana na watu wenye tabia hizo, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola.

Aidha Kamanda Fuime ametoa mwito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuwezesha kupatikana na kukamatwa kwa watu hao na wahalifu wengine.

No comments:

Post a Comment