SERIKALI imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka
Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa
mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka
mitano.
Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha
Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye
anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.
Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika
leo (Ijumaa, Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na
Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha
uchunguzi huo.
“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili
kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi
uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi
ziendelee,” alisema.
Waziri Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya
TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa
walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na ikithibitika hawakuhusika basi
watarudishwa.
Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia
flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara
moja.
Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara
kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha
akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo
zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).
Pia Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta
yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya
kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko
Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx
Energies.
Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER
imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta
linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo
litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Jana niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja
ili kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia
wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021, 11410 DAR ES SALAAM.
IJUMAA, FEBRUARI 12, 2016.
No comments:
Post a Comment