Friday, March 03, 2017

RAIS DKT. MAGUFULI ATOA MIEZI MINNE MRADI WA MAJI WA NG’APA MKOANI LINDI UKAMILIKE PIA AKUTANA NA BODI YA WAKURUGENZI WA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (AfDB) KATIKA IKULU NDOGO YA LINDI.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Waziri wa Maji Mhandisi Gerson Lwenge kuhakikisha kuwa Mradi wa Maji wa Ng’apa uliopo mkoani Lindi unakamilika ndani ya miezi mine na si vinginevyo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mama Salma Kikwete mara baada ya kuwasalimia wananchi waliokusanyika karibu na mradi wa Maji wa Ng’apa uliopo Mkoani Lindi. Pia Mama Salma Kikwete amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Mbunge mteule Mama Salma Kikwete mara baada ya kuwasalimia wananchi waliokusanyika karibu na mradi wa Maji wa Ng’apa uliopo Mkoani Lindi.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Ng’apa mara baada ya kutembelea mradi wa Maji wa eneo hilo ambao unasuasua kukamilika. Rais Dkt. Magufuli ametoa miezi minne kwa Mkandarasi kampuni ya Overseas Infrastructure Alliance Private Limited ya India kuhakikisha kuwa inakamilisha ujenzi wa mradi huo na sio kuleta visingizio.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ikulu ndogo Mkoani Lindi.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Ikulu ndogo Mkoani Lindi. Wakwanza kushoto ni Kiongozi wa Wakurugenzi hao Lekhethe Mmakgoshi kutoka Nchini Afrika Kusini na Wakwanza kulia ni Mkurugenzi mwingine wa (AfDB) Dkt.Nyamajeje Weggoro ambaye ni Mtanzania.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Kiongozi wa Wakurugenzi hao kutoka (AfDB) Lekhethe Mmakgoshi mara baada ya kumaliza mazungumzo na Bodi hiyo ya Wakurugenzi.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Mmoja wa Wakurugenzi wa (AfDB) Dkt.Nyamajeje Weggoro mara baada ya kumaliza mazungumzo na Bodi yao Ikulu ndogo mkoani Lindi.
Sehemu ya Mradi wa Maji wa Ng’apa mkoani Lindi ambao Rais Dkt. Magufuli ametoa miezi minne kwa mkandarasi anayejenga mradi huo ili uweze kukamilika haraka.
PICHA NA IKULU
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

Simu : +255-22-2114512, 2116898
Email : press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India Bw. Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo itakapokamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 03 Machi, 2017 alipotembelea mradi huo ambao unatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.
Mhe. Dkt. Magufuli ameelezea kusikitishwa na usimamizi mbaya wa mradi huo ambao tayari kiasi cha Shilingi Bilioni 21.8 zimetolewa kati ya Shilingi Bilioni 29 zilizopangwa kutumika hadi kukamilika kwake, na ameonya kuwa endapo mradi huo hautakamilika katika kipindi cha miezi 4 kuanzia sasa atachukua hatua dhidi ya wanaopaswa kuusimamia.
"Ikipita miezi minne nisilaumiwe, hatuwezi kukubali wananchi wa Lindi wanashida ya maji, fedha zimetolewa, mkandarasi anaamua kupeleka fedha India, mradi umecheleweshwa kwa miaka miwili na mkandarasi hayupo kwenye eneo la ujenzi halafu mnaopaswa kumsimamia mnamuangalia tu wakati sheria zipo, kwa nini hamkumfukuza muda wote huu?" amehoji Mhe. Rais Magufuli.
Mapema akitoa maelezo kuhusu mradi huo Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amesema mradi huo unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambapo hadi sasa umefikia asilimia 85 na kwamba mkandarasi amesimamisha kazi kutokana na kuishiwa fedha.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na ameiomba bodi hiyo ishirikiane na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa "Standard Gauge".
Pamoja na kutoa ombi hilo Mhe. Dkt. Magufuli ameipongeza benki hiyo kwa kutoa mikopo nafuu iliyowezesha kutekelezwa kwa miradi mingi ya maendeleo hapa nchini hususani ujenzi wa barabara lakini ameomba mchakato wa upatikanaji wa mikopo hiyo urahisishwe na kuharakishwa ili miradi mingi zaidi itekelezwe kwa wakati.
"Hapa Tanzania AfDB imefanya mambo makubwa sana, tunaipenda sana benki hii kwa sababu imetuwezesha kujenga barabara nyingi zikiwemo ya Iringa - Dodoma inayounganisha Cape Town Afrika Kusini hadi Misri, barabara ya Namtumbo - Tunduru - Masasi na nyingine nyingi, kwa kweli hawa ni wadau muhimu wa maendeleo" amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akizungumza baada ya kikao hicho kiongozi wa Bodi ya Wakurugenzi waliokutana na Mhe. Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Lindi Bi. Lekhethe Mmakgoshi amempongeza Mhe. Dkt. Magufuli kwa juhudi zake za kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania na ameahidi kuwaAfDB itaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania ikiwemo kufanyia kazi  maombi aliyoyatoa kwa Bodi hiyo.
Nae Dkt. Namajeje Weggoro ambaye ni mmoja wa wakurugenzi hao anayewakilisha nchi saba za Afrika ikiwemo Tanzania amesema Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kupata mikopo mingi kutoka AfDB na ameongeza kuwa maombi yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli yatapewa kipaumbele.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Lindi
03 Machi, 2017

No comments:

Post a Comment