Chama cha Madaktari wa Kenya (KMPDU), kimewataka wenzao wa Tanzania wasikubali kusaini mkataba wowote wa kwenda Kenya kabla mgogoro wao na Serikali haujatatuliwa.
Taarifa ya KMPDU inasema haina tatizo na uwezo ama mafunzo ya madaktari wa Tanzania na protokali ya leseni za madaktari inayotambulika na Baraza na Bodi za nchi za Afrika Mashariki.
“Lakini tunapenda kuwataarifu kwamba kwa miaka miwili iliyopita, madaktari wa Kenya wamekuwa wakihangaika na Serikali ya Kenya kuhusu idadi yetu na kukataliwa kwa kile Serikali na Wizara ya Afya ilichosema ni ukomo wa bajeti jambo ambalo lilikuwa likichochea mgomo uliokwisha wiki moja iliyopita.
“Tunawashukuru kwa kutuunga mkono wakati wa mgomo wetu uliodumu kwa siku 100.
“Tumeona makubaliano ya Serikali ya Kenya na Tanzania wa kuleta madaktari 500 ili kuleta uwiano (ration) kati ya wagonjwa na madaktari kwenye pengo lililopo nchini kwa sasa.
“Hadi kufikia Mei 2017, kutakuwa na madaktari wanaokadiriwa kufikia 1,400 ambao hawajaajiriwa na Serikali ya Kenya,” ilisema taarifa hiyo.
Wakati huo huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema madaktari 159 nchini wametuma maombi ya kazi kwenda kufanya kazi nchini Kenya hadi sasa, tangu Serikali ilipotoa tangazo Machi 18, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ummy aliwatoa hofu madaktari kuhusu usalama wao wawapo nchini Kenya kutekeleza majukumu yao.
“Rais Uhuru Kenyata ambaye ni mwenyeji wetu, amemuhakikishia Rais Dk. John Magufuli, kwamba tutakuwa salama,” alisema.
Ili kukamilisha suala hilo, alisema tayari wizara yake imeandaa rasimu ya makubaliano ambayo itaeleza mambo yote kimaandishi, likiwamo suala la usalama na masilahi yao waliyoahidiwa.
Alisema madaktari hao watakapoajiriwa nchini humo watalipwa mshahara sawa na madaktari wengine wa huko.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Bakari, alisema kabla ya uamuzi huo kutolewa na kukubaliwa na nchi zote mbili, ulijadiliwa kwa kina faida na athari zitakazojitokeza.
“Kenya ilituhakikishia usalama wa madaktari wetu, mshahara mzuri pamoja na makazi ya uhakika, hivyo Serikali ilijiridhisha ni fursa nzuri ya ajira kwa madaktari wetu,” alisema Profesa Mohamed.
Msimamo wa MAT
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimepinga uamuzi wa Serikali kuipatia madaktari 500 Kenya hadi hapo nchi hiyo itakapoanza kutekeleza makubaliano kati yake na madaktari wake ambao hivi karibuni waligoma kwa takribani miezi mitatu.
Taarifa ya MAT iliyotolewa juzi na Mwenyekiti wake, Dk. Obadia Nyogole, ilisema: “Kumekuwepo na maoni tofauti juu ya madaktari wa Tanzania kwenda Kenya, na zaidi ya asilimia 60 ya madaktari wa nchi hiyo wamepinga suala hilo na kutaka wazawa kwanza ndiyo waajiriwe.
No comments:
Post a Comment