TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU GHARAMA ZA MATIBABU YA DAWA YA SUMU YA NYOKA NCHINI
Kama
tunavyofahamu, nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi wakimuuma mtu
huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu kwamba tatizo hili lipo
zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa wananchi kumudu gharama za
matibabu ni mdogo.
Dawa za kutibu
sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi. Dawa hizo siyo tu hazipatikani kwa
urahisi, bali pia zinapatikana kwa
gharama kubwa. Bei ya
kununulia dawa hizi ni kati ya dola za kimarekani 55 hadi 85 (yaani shilingi za
kiTanzania 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo (vial) kimoja. Kichupa hicho
huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini mara
tu baada ya kufunguliwa dawa hiyo
huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi mmoja tu.
Pamoja
na changamoto hizo, Serikali kupitia MSD kila mwaka huagiza dawa hizi kwa ajili
ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni TZS
200,000/= kwa kichupa kimoja. Hospitali
zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa washitiri
wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika wanaohitaji dawa za sumu za
nyoka mara zinapohitajika.
Napenda
kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za tiba hutolewa
bure kwa makundi maalum, au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya gharama, au kwa
kupitia mfumo wa Bima mbalimbali za Afya kama vile CHF. Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu
wa msamaha hutumika.
Katika
kuhakikisha kwamba wananchi wanaohitaji dawa ya
sumu ya nyoka wanahudumiwa ipasavyo, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anatoa maelekezo yafuatayo:-
1.
Waganga
Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Hospitali zote nchini wahakikishe kuwa Hospitali
zote za umma zinaingiza dawa hii katika
dawa za dharura ili iweze kununuliwa kama dawa zingine za dharura kupitia
kifungu cha fedha za dawa za dharura.
2.
Kwa wagonjwa
ambao watakuwa na Bima ya Afya, basi gharama za matibabu hayo zitalipwa kwa
kupitia utaratibu huo wa Bima. Wananchi wanahimizwa kujiunga na Bima za Afya
(CHF/NHIF) ili kupata unafuu wa matibabu haya na mengine. Mfano CHF - gharama
ya kujiunga katika Halmashauri mbalimbali kwa kaya ni kati ya shilingi 5,000/=
hadi shilingi 30,000/= kwa mwaka.
3.
Kwa
wagonjwa ambao watakuwa hawana Bima ya Afya, hao watatakiwa kuchangia gharama
hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya
dawa hizi au kwa kiwango kingine kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali
kadri itavyohitajika. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba kung'atwa na
nyoka ni ajali na wananchi wengi wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya
vijijini ambao kimsingi uwezo wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya
dawa ya sumu ya nyoka ni mdogo.
4.
Wagonjwa
watakaothibitika kuwa hawana fedha za kuchangia gharama hiyo, basi hospitali
husika kwa kupitia mpango wa msamaha wa kulipia huduma za afya wahakikishe
kwamba wanampatia mgonjwa huduma hizo kwa utaratibu wa msamaha wa gharama hizo.
Aidha, kwa
kuwa nchi yetu ni kubwa na ina nyoka wengi, Mhe Waziri wa Afya anawaagiza
Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kupitia kwa uangalifu takwimu za wagonjwa walioumwa na nyoka katika
kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 na kuziwasilisha Wizarani
kabla ya tarehe 31 Januari 2017 ili kupata takwimu za mahitaji halisi ya dawa ya
sumu ya nyoka nchini. Hii itasaidia
kuboresha upangaji, uagizaji na upatikanaji wa dawa hizo nchini.
Vile
vile, Waziri wa Afya ameiagiza Bohari ya Dawa (MSD) kuweka utaratibu wa haraka wa kununua dawa hizo moja
kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa bei.
Imetolewa na:-
Catherine Sungura
Msemaji wa Wizara - Afya
26/12/2016
No comments:
Post a Comment