Wednesday, February 22, 2017

WATATU WAPOTEZA MAISHA AKIWEMO OC CID KIBITI PETER KUBEZYA

RPC
KAMANDA wa polisi mkoani Pwani, Boniventure  Mushongi, akizungumzia tukio la  mauaji lililotokea wilayani Kibiti mkoani Pwani.

Watu watatu wamepoteza maisha mmoja kati yao akiwa OC CID Kibiti baada ya kuuwawa na  kundi la watu wanaodhaniwa ni majambazi wakiwa na silaha aina ya SMG/SAR huko eneo la Jaribu Mpakani kata ya Majawa ,Kibiti .
Tukio hilo limetokea feb 21 majira ya saa  mbili usiku  ambapo  watu sita  walivamia katika kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu na kuuwa watu watatu .
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi alithibitisha kutokea  kwa tukio hilo ,aliwataja  waliouawa kuwa ni OC CID wilaya ya Kibiti sp.Peter Kubezya ambae amepigwa risasi kwenye kiuno .
Wengine  ni Peter Kitundu Mkaguzi wa maliasili kituo cha Jaribu  Mpakani na mgambo  aliyekuwa akifanyakazi za ulinzi kwenye kizuizi hicho, Athumani Ngambo .
Kamanda Mushongi alisema wote hao wawili waliuawa kwa kupigwa  risasi kichwani na begani na kupoteza maisha papo hapo .
Aidha wakati majambazi hayo yakifanya uhalifu huo waliweza kuwaita wananchi wafike kwenye kizuizi hicho ili wachukue mkaa na mazao ya misitu  .
Kufuatia  wito huo wananchi walijitokeza na kwenda kujibebea mkaa na mazao hayo kisha kuondoka  nayo.
“Baada ya kutokea  kwa tukio hilo kundi la  makachero likiongozwa na OC CID Kubezya lilifika eneo la  tukio kupambana na wahalifu lakini wakiwa kwenye majibizano ya kurushiana risasi mkuu huyo wa upelelezi alijeruhiwa kiunoni ambapo alifariki akiwa njiani akielekea hospitali  ya mission ya Mchukwi ” alieleza Mushongi .
Kamanda Mushongi alifafanua kwamba katika eneo la  tukio kulikutwa pikipiki mbili namba  MC 853 AHH aina ya Toyo na MC 799 aina ya Sunlg pamoja na kipeperushi chenye ujumbe wa kitisho .
Kutoka vyanzo mbalimbali huko Kibiti vinasema vipeperushi hivyo vinaeleza kupinga kuwepo kwa vizuizu  vya mazao ya misitu  wilayani humo.

No comments:

Post a Comment