Askofu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu WAPO MIssion International.
Wiki iliyopita tulifanya uchambuzi wa fungu la karama za NGUVU ambazo ni karama ya Imani, Matendo ya miujiza na karama za kuponya magonjwa. Leo tunahitimisha kipengele hiki kwa kuchambua fungu la mwisho la karama za MAWASILIANO ambazo ni karama ya unabii, aina za lugha na tafsiri za lugha:
Tafsiri ya Karama ya unabii
Fungu la karama za mawasiliano ambazo ni “karama ya unabii”; “karama ya aina za lugha” na “karama ya tafsiri za lugha” Nitaanza na “karama ya unabii.” Kwanza kabla ya kutafsi karama tuanze na msamiati wa neno “unabii” kwa mujibu wa Biblia. “unabii” ni ujumbe maalum kutoka kwa Mungu, ukiletwa na Roho Mtakatifu na kufunuliwa kwa mpokeaji/nabii/mtu aliyeteuliwa kwa wakati huo kuuwasilisha ujumbe huo kwa walengwa.
Ujumbe huu wa kinabii unapotangazwa na msemaji aliyeupokea, lazima uwasilishwe kwa lugha inayojulikana na wasikilizaji. Lazima ujumbe huo uwe umebeba taarifa ambazo mlengwa akiusikia atajitambua kuwa ujumbe huo ni wa kwakwe. Kwa maelezo mengine, unabii ni ujumbe wa Mungu kupitia kwa mpokeaji ili auwasilishe kwa walengwa pasipo yeye kuingiza mawazo yake ya kibinandamu.
Sasa tuje kwenye tafsiri ya “karama ya unabii”. Tafsiri nyepesi kueleweka kwa wazi zaidi ni “mpokeaji kupokea “zawadi ya kutumika kuwasilisha ujumbe kutoka kwa Mungu kwa ajili ya kuwajenga, kuwafariji na kuwatia moyo walengwa wa unabii huo; “Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, kuwafariji, na kuwatia moyo.” (1 Kor.14:3)